SYRIA

Wapiganaji wa jeshi huru la Syria watumia mwanya wa kuweka silaha chini kujikusanya upya

Baadhi ya wapiganaji wa jeshi huru la Syria
Baadhi ya wapiganaji wa jeshi huru la Syria Reuters

Wakati pande mbili zinazopigana nchini Syria zikiwa zimesitisha mapigano kwa muda kuridhia mapendekezo ya msuluhishi mkuu wa mgogoro huo Koffi Annan, imeelezwa kuwa wapiganaji wa jeshi huru la Syria wanaendelea kujikusanya.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa za wapiganaji hao kuanza kujikusanya tena zimekuja kufuatia taarifa ya habari ya kituo kimoja cha kimataifa ambacho kimefanya mahojiano na viongozi wa kijeshi wa jeshi huru la Syria ambao wamekiri kutumia muda huu kujikusanya.

Mmoja wa viongozi wa wapiganaji hao amesema kuwa wanatumia muda huu ambapo wanatii mapendekezo ya kusitisha mapigano kwa lengo la kutafuta suluhu kuanza kujikusanya upya kwakuwa wanaamini serikali yao itawashambulia hivi karibuni.

Wapiganaji hao licha ya kutangaza kuweka silaha zao chini, wameonekana katika makundi wakiendelea kujikusanya huku wengine wakisaidiwa kwa silaha hali inayooashiria kuwa hawakutaka kusalimisha silaha zao.

Wanajeshi wa Syria wengi wameondoka kwenye miji ambayo walikuwa wanakalia huku waangalizi wa Umoja wa Mataifa walioko nchini humo wakisema kuwa kwa kiasi kikubwa mapendekezo ya Koffi Annan yameanza kutekelzwa kikamilifu.

Lakini wakati wanajeshi hao wakijikusanya, nchi hiyo jana imefanya uchaguzi mkuu wa wabunge uchaguzi ambao ulimalizika salama licha ya baadhi ya vyama vya upinzani kususia uchaguzi huo wakidai haukuwa huru na haki.

Uchaguzi huo umefanyika kufuatia serikali kuitisha kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba na kuruhusu mfumo wa vyama vingi na huu ukiwa ni uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia.