ISRAEL

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akubali kuunda Serikali ya muungano na chama cha Kadima

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu
Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu Reuters

Ikiwa ni siku mbili zimepita toka waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu atangaze kuitisha uchaguzi mkuu mapema zaidi nchini humo, chama chake kimelazimika kuungana na chama kikuu cha upinzani cha Kadima.  

Matangazo ya kibiashara

Chama cha Kadima kimekubali kuingia kwenye serikali ya waziri mkuu Netanyahu kwa lengo la kushirikiana kupitisha baadhi ya sheria ambazo awali vyama vingine vya upinzani vilikuwa vinapinga.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo ni kwamba kiongozi wa Kadima, Shaul Mofaz atakuwa naibu waziri mkuu na pia waziri ambaye hana wizara maalumu kwenye serikali ya Umoja.

Hata hivyo taarifa kutoka kwenye vyama vyote viwili bado hazijaweka wazi malengo ya makubaliano hayo ingawa vimethibitisha kukubaliana kuungana katika kutimiza baadhi ya malengo ya serikali.

Hata hivyo makubaliano hayo yamelaaniwa vikali na kiongozi wa chama cha Meretz, Zehava Galon ambaye amesema kuwa uamuzi huo unashangaza na ni dhahiri yanalenga kudumaza demokrasia nchini humo.

Serikali ya waziri mkuu Netanyahu juma hili ilitangaza kuitisha uchaguzi mkuu mapema zaidi ambapo imepanga kufanya uchaguzi huo ifikapo september 4 mwaka huu.

Hata hivyo ili muungano huo uweze kuanza ni lazima bunge la nchi hiyo lipige kura kukubali ama kukataa serikali ya Umoja jambo ambalo linawezekana likakataliwa bungeni.