LIBYA

Al Keib: Waliovamia ofisi ya waziri mkuu hawakuwa wapiganaji walioshiriki mapinduzi ya Libya

Waziri mkuu wa Libya Abdulrrahim al-Keib
Waziri mkuu wa Libya Abdulrrahim al-Keib Reuters

Waziri mkuu wa Libya Abdulrrahim al-Keib amesema kuwa watu waliovamia ofisi yake jana mchana hawakuwa wapiganaji walioshiriki mapinduzi nchini humo bali amewaita ni kikundi cha majambazi.

Matangazo ya kibiashara

Kauli hiyo ameitoa ikiwa zimepita saa chache toka kundi la watu waliokadiriwa kufikia 200, kuvamia ofisi za waziri mkuu wakitaka kupewa malipo yao ambayo walidai ni ya kushiriki vita vya kumng'oa aliyekuwa mtawala wa nchi hiyo Kanali Muamar Gaddafi.

Watu hao wakiwa na risasi pamoja na mabomu walianza kurusha risasi kuelekea jengo la waziri mkuu ambapo waliua askari mmoja kabla ya kuondolewa na vikosi vya Serikali vilivyofika eneo la tukio.

Shambulio hilo limekuwa ni mfululizo wa mashambulizi ambayo yanatekelezwa nchini humo na watu wanaodai kuwa ndio walioshiriki kikamilifu kuuangusha utawala wa Gaddafi lakini wamekuwa wakisahaulika.

Waziri mkuu Keib amesema kuwa malipo kama zawadi kwa wapiganaji walioshiriki kuuondoa utawala wa Gaddafi yatafanyika kama Serikali ilivyoahidi na kwamba haina haja ya wapiganaji hao kuingia kwenye vurugu kushinikiza kulipwa pesa hizo.