SYRIA-UN

Annan: Nchi ya Syria hatarini kuingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe

Msafara wa magari ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa walioko nchini Syria wakiwa kwenye mji wa Homs
Msafara wa magari ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa walioko nchini Syria wakiwa kwenye mji wa Homs UN Photo/Nadine Kaddoura

Msuluhishi mkuu wa mgogoro wa Syria, Koffi Annan ameonya nchi hiyo kuingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na mashambuliziya mabomu ya kujitoa muhanga yanayoendelea kutekelezwa nchini Syria.

Matangazo ya kibiashara

Akihutubia mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa kupitia video akiwa nchini Uswis, Annan amewaambia wajumbe wa mkutnao huo kuwa licha ya hali kuwa tulivu nchini Syria lakini kumekuwa na vitendo vya uvunjifu wa amani kwenye baadhi ya maeneo.

Annan amesema kuwa, watu wasiojulikana wamekuwa wakiendesha mashambulizi ya kujitoa muhanga kwenye miji ya Homs na Damascus mashambulizi ambayo yanaelezwa kufanywa na wapiganaji wa jeshi huru la Syria wakishirikiana na makundi ya kigaidi.

Mbali na kulaani mashambulizi hayo, msuluhishi huyo pia ameonya dhidi ya kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo kutokana na mashambulizi ambayo yameendelea kutokea katika baadhi ya maeneo kati ya wanajeshi wa Serikali na wale wa jeshi huru la Syria.

Kiongozi huyo amedai kuwa endapo vita hivyo havitazuiliwa mapema, basi haitakuwa na madhara kwa wananchi pekee wa Syria bali vitasambaa hadi kwenye eneo zima la ukanda wa mashariki ya kati hasa kwenye ambazo zinaizunguka Syria.

Mapigano hayo yameripotiwa licha ya uwepo wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini humo ambao wanasimamia kusitishwa kwa mapigano ambapo kunatarajiwa kuwasili kwa zaidi ya waangalizi 300 wa Umoja huo nchini Syria.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanadai kuwa zaidi ya watu elfu kumi wameuawa toka kuanza kwa harakati za kutaka kuipindua Serikali ya rais Bashar al-Asad.