MAREKANI

Rais Barack Obama atangaza kuunga mkono ndoa za watu wa jinsia moja

Rais wa Marekani Barack Obama
Rais wa Marekani Barack Obama REUTERS/Larry Downing

Katika kile kinachoonekana ni kutafuta uungwaji mkono kwenye uchaguzi mkuu uajo nchini Marekani, rais Barack Obama ametangaza rasmi kuunga mkono ndoa za jinsia moja akisema kuwa nao wana haki kama binadamu wengine.

Matangazo ya kibiashara

Kauli ya rais Obama imeungwa mkono na makundi ya wanaharakati na watu wanataka kuruhusiwa kwa ndoa za jinsia moja nchini Marekani, kauli ambayo imeelezwa kulenga kuua nguvu ya upinzani toka chama cha Conservative.

Tayari kumeibuka mitazamo tofauti kuhusu msimamo wa rais Obama kwenye suala la ndoa ya jinsia moja ambapo makundi mengine ya wanaharakati wamekosoa kauli ya Obama ambaye awali alikuwa haungi mkono ndoa za jinsia moja.

Mkurugenzi mtendaji wa taasisi inayosimamia haki za Mashoga na wasagaji ya National Gay and Lesbian Task force amempongeza na kumsifu Obama kuwa Rais wa Kwanza kuunga mkono ndoa za namna hiyo nchini Marekani.

Rais wa chama kinachopinga ndoa za jinsi moja Brian Brown amesema kuwa Obama ameitoa hoja hiyo ikiwa ni ajenda katika kampeni zake na harakati za uchaguzi wa Urais zijazo.

Obama amesema kuwa Serikali yake haina sababu ya kuweka vikwazo kwa watu waliokuwa katika mahusiano ya jinsia moja na kwamba wana haki kama wanandoa wengine.

Majimbo kadhaa nchini Marekani yamepitisha na kukubali ndoa za jinsia moja huku majimbo mengine yakipitisha sheria ya kutoruhusu ndoa hizo.