INDONESIA

Waokoaji nchini Indonesia wabaini eneo ambalo ndege iliyopotea ilianguka, juhudi za kufika eneo la tukio zinaendelea

Eneo ambalo ndege ya Indonesia inaelezwa kuanguka
Eneo ambalo ndege ya Indonesia inaelezwa kuanguka Reuters

Kikosi cha waokoaji nchini Indonesia hii leo kimegundua mabaki ya ndege ya urusi aina ya Sukhoi Superjet iliyopoteza mawasiliano na kupotea muda mchache mara baada ya kuruka toka kiwanja cha ndege nchini humo ikiwa na abiria 50.

Matangazo ya kibiashara

Ndege hiyo ilitoweka na kupoteza mawasiliano kusini mwa mji wa Jakata nchini Indonesia hapo jana, ikiwa ni dakika 50 toka iruke kwa kile kilichoelezwa kuwa ilikuwa ikifanya safari fupi ya kuonesha uwezo wake kwa wateja.

Juhudi za awali za kuitafuta ndege hiyo hazikuzaa matunda na baada ya kurejea kuisaka ndege hiyo Rubani wa Helkopta aligundua kuwa kuna mabaki ya ndege hiyo katika maeneo ya mlimani.

Msemaji wa Operesheni iliyotekelezwa na jeshi la anga, amesema ndege hiyo iligundulika katika eneo la Cirjuk karibu na mlima Salak karibu na mji wa Bogor, JAVA Magharibi.

Hata hivyo bado mamlaka nchini humo hazijathibitisha kama mabaki yaliyopatikana ni ya ndege hiyo wala kubaini endapo kuna manusura wowote wa ajali hiyo.

Polisi wa uwanja wa ndege wa Indonesia wanaendelea na uchunguzi kuhusu chanzo cha ndege hiyo kupoteza mawasiliano ingawa waongoza ndege wa uwanja wa ndege wa Indonesia wamesema kuwa rubani wa ndege hiyo mara ya mwisho alisikika akiomba kubadili uelekea na kupunguza umbali wa kuruka ndege hiyo na ndipo walipopoteza mawasiliano.

Tayari vikosi vya ukoaji vya Indonesia na wale toka nchini Urusi wamewasili kwenye eneo la tukio kuendelea na uchunguzi zaidi ikiwemo kukisaka kisanduku cheusi cha sauti kubaini chanzo hasa ambacho pengine ndicho kilichosababisha ajali hiyo.