SYRIA-DAMASCUS

Watu zaidi ya 50 wauawa katika milipuko miwili ya bomu iliyotokea mjini Damascus, Syria

Watu zaidi ya hamsini wameripotiwa kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya wengi wao wakiwa ni wanafunzi kwenye mashambulizi mawili tofauti ya mabomu iliyotokea kwenye mji mkuu wa Syria, Damascus 

Magari yakionekana kuwaka moto mjini Damascus mara baada ya shambulio la hii leo
Magari yakionekana kuwaka moto mjini Damascus mara baada ya shambulio la hii leo Reuters
Matangazo ya kibiashara

Mashambulizi hayo mawili ambayo yameelezwa kuwa ni makubwa zaidi kuwahi kutekelezwa nchini humo toka kuanza kwa harakati za kutaka kuuondoa utawala wa rais Asad madarakani.

Shambulio hilo limetokea wakati ambapo raia wa Syria walikuwa wakielekea kwenye kazi zao ambapo wakati mlipuko huo unatokea wanafunzi ndio waliokuwa wengi wakielekea shuleni.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amelaani vikali shambulio la bomu lililotekelezwa kwenye mji mkuu wa Syria Damascus pamoja na miji mingine ambayo imekumbwa na milipuko.

Shambulio la mjini Damascus limekuja ikiwa zimepita saa chache toka msafara wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa walioko nchini humo kunusurika kwenye shambulio la roketi lililovurumishwa kwenye gari la askari ambao walikuwa wanawasindikiza waangalizi hao.

Shambulio hilo lilitokea kwenye mji wa Homs wakati waangalizi wa Umoja wa Mataifa wakiingia kwenye mji huo wakiongozwa na wanajeshi wa Serikali ambao wamekuwa wakiandamana na msafara wa waangalizi hao kwenye miji mbalimbali nchini humo.

Shambulio la mjini Damascus limezua hofu kwa wananchi wa mji huo ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakilengwa na mashambulizi ya mabomu ambayo yanatekelezwa na watu wasiofahamika.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa mashambulizi yanayoendelea yanadhihirisha kuwa badio hali ya mambo nchini Syria haijatengamaa na kuwaonya waasi ambao wanapigana na serikali, waasi ambao ndio wametuhumiwa kutekeleza mashambulizi hayo.

Rais Bashar al-Asad ameonya makundi ambayo yanapigana na serikali na kuongeza kuwa kamwe Serikali haitavumilia kuona watu wachache wakitaka kuibomoa nchi hiyo na hivyo hatua mathubuti zitachukuliwa kukabiliana na wapiganaji hao.

Hapo jana upinzani nchini humo umesema kuwa vitendo vya mashambulizi vinafanywa na serikali kwa lengo la kutaka kuonyesha dunia kuwa upinzani ndio unatekeleza mashambulizi hayo ili kupata mwanya wa kuendeleza visa vyao vya unyanyasaji.