MISRI-CAIRO

Wagombea wawili wa urais nchini Misri washutumiana wakati wa wakishiriki mdahalo wa Televisheni

Abdel Moneim Abu Futuh (kushoto) pamoja na Amr Moussa (kulia) wakiwa kwenye mdahalo wa Televisheni
Abdel Moneim Abu Futuh (kushoto) pamoja na Amr Moussa (kulia) wakiwa kwenye mdahalo wa Televisheni Reuters

Wagombea wawili kati ya kumi na tatu wanaowania urais nchini Misri hapo jana walipambana vikali kwenye mdahalo wa kwanza uliorushwa kwa njia ya Televisheni na kushuhudiwa na maelfu ya wananchi wa Misri na nchi Jirani.

Matangazo ya kibiashara

Viongozi hao wawili ambao wanapewa nafasi kubwa ya kuweza kupata nafasi ya kuongoza nchi hiyo ni pamoja na aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje wakati wa utawala wa rais Hosni Mubarack, Amr Moussa na daktari maarufu na mmoja wa wanachama wenye nyadhifa ya juu ndani ya chama cha Muslim Brotherhood, abdel Moneim Aboul Fotouh.

Mdahalo huo wa urais ambao ni wa kwanza kufanyika nchini huko katika kipindi cha miaka 30 toka kumalizika kwa utawala wa Mubarak, mdahalo huo ulidumu kwa muda wa saa nne.

Mdahalo huo ulishika kasi na kila mgombea kuanza kurusha maneno makali na ya kejeli dhidi ya mgombea mwenzake wakati Moussa alipomtuhumu Fotouh kiongozi wa chama cha Muslim Brotherhood kuandika barua za kichochezi zinazotaka kuibadilisha nchi hiyo kuwa ya kiislamu.

Kufuatia matamshi hayo, Fotouh nae aliamua kujibu mashambulizi baada ya uvumilivu kumshinda na kumtuhumu mwenzake kuwa wakati wa utawala wa Mubarak alikuwa kinara wa kutekeleza kile ambacho alikuwa akiagizwa kufanya na rais Mubarak na kwamba alishindwa kushiriki mapinduzi ya kuung'oa utawala wa bosi wake.

Viongozi hao wanatarajiwa kuchuana kwenye uchaguzi mkuu wa urais uliopangwa kufanyika tarehe 23 na 24 ya mwezi huu, uchaguzi ambao umegubikwa na mizengwe mingi kufuatia mahakama moja hivi karibuni kutangaza kusitisha uchaguzi huo.

Wagombea wengine wanaopewa nafasi ni pamoja na mgombea mwingine toka chama cha Muslim Brotherhood Mohammed Morsi, wengine ni Hamdeen Sabahi, mbunge wa chama cha Dignity a Nasserist na mwanasheria wa haki za binadamu Khaled Ali.