Watu 41 wajeruhiwa nchini Guinea kufuatia maandamano yaliyoitishwa na upinzani
Watu zaidi ya arobaini na moja wamejeruhiwa vibaya nchini Guinea kufuatia makabiliano kati ya polisi na waandamanaji waliokuwa wanapinga kucheleweshwa kwa uchaguzi wa wabunge nchini humo.
Imechapishwa:
Watu kadhaa wameripotiwa kupigwa risasi za moto na polisi wakati wa maandamano hayo, huku polisi nao wakidai zaidi ya askari wake kumi na saba nao wamejeruhiwa vibaya na wananchi walioshiriki maandamano ya hapo jana.
Akizungumza kupitia kituo cha televisheni ya taifa nchini humo, waziri wa mambo ya ndani wa Guinea, Alhassane Conde ametishia Serikali kuwachukulia hatua wale wote ambao wataendelea na maandamano hii leo na kusema kuwa atakayefanya hivyo atakuwa ameenda kinyume na sheria za nchi.
Maandamano hayo yamefanyika hapo jana kufuatia wito wa viongozi wa vyama vya upinzani nchini humo, siku ya Jumatatu kutangaza kuitisha maandamano ya nchi nzima kushinikiza kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa wabunge.
Upinzani ulisema kuwa siku ya Alhamisi ndio siku ambayo maandamano yaliyoitishwa yataanza kutekelezwa na kuendelea mpaka pale Serikali itakapotangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Hivi karibuni rais Alpha Conde alitangaza kusogeza mbele kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa wabunge nchini humo kwa kile alichoeleza ni kutokamilika kwa maandalizi ya uchaguzi huo.
Viongozi wa upinzani wanadai kuwa lengo la Serikali kuchelewesha uchaguzi huo ni kwasababu rais Conde na chama chake wanajua hawatashinda kihalali kwahivyo wanataka kutumia mwanya wa kuhakiki daftari la wapiga kura ili kuiba kura za wananchi.
Uchaguzi huo ulikuwa umepangwa kufanyika katika kipindi cha miezi sita toka kuingia madarakani kwa utawala wa kiraia na kumalizika kwa utawala wa kijeshi kwa mujibu wa katiba na tume ya utangamano iliyoundwa kusimamia zoezi hilo.
Rais Conde ameahidi uchaguzi huo kufanyika tarehe 8 ya mwezi wa saba.