MAREKANI

Viongozi wa NATO wakubaliana kuondoa majeshi nchini Afganistan

REUTERS/Yves Herman

Nchi za Jumuiya ya Kujihami ya nchi za magharibi, NATO wameunga mkono mpango wa kuondoa majeshi yake nchini Afghanistan ifikapo mwaka 2014 na hivyo kuhitimisha operesheni ya kijeshi nchini humo.  

Matangazo ya kibiashara

Mpango huo unalenga kukabidhi jukumu hilo la ulinzi na usalama mikononi mwa majeshi ya Afghanstan kuanzia katikati ya mwaka ujao wa 2013 ingawa viongozi hao wamesema lazima kuwe na mpango wa kuisadia nchi hiyo.

Katika mkutano huo wa NATO uliofanyika Chicago nchini Marekani, Rais Barack Obama amesema muungano huo wa majeshi ya NATO umekubaliana kutekeleza mpango huo wa kuondoa majeshi hayo nchini Afghanistan.

Rais Obama amesema kuwa NATO imekubaliana kuuondoa wanajeshi wake wapatao 130,000 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2014 kwa kufuata misingi ya makini na uwajibikaji.

Aidha viongozi hao wa NATO wamewaagiza maafisa wa kijeshi kuanza kupanga mpango mpya ambao utaisaidia Afghanistan baada ya majeshi yote ya NATO kuondoka nchini humo.

Wamesema kuwa mpango huo huo ni vema ukaangalia maeneo ya mafunzo, ushauri na kuyasaidia majeshi ya Afghanistan kuisaidia serikali imudu kukabiliana na kundi la Taliban.

Kwa upande wake Obama ameendelea kusisitiza kuwa Afghanistan haitaachwa peke yake na kuhakikisha muongo wa vita ambao umesababisha vifo vya wanajeshi wa NATO wapatao 3,000 na maelfu ya wanajeshi wa Afghanistan.