IRAN-IRAQ

Mazungumzo ya nyuklia kuhusu Iran yaingia siku ya pili

REUTERS/Government Spokesman Office/Handout

Mazungumzo yaliyolenga kusaidia kufikia muafaka wa mgogoro wa muda mrefu kuhusu mpango wa Nyuklia wa Iran umeingia katika siku ya pili hii leo mjini Baghdad nchini Iraq. Katika mkutano huo hapo jana mataifa sita yenye nguvu duniani, Uingereza, China, Ufaransa, Urusi, Marekani na Ujerumani yaliweka mapendekezo mapya mezani hatua ambayo imeUogopesha upande wa Iran.

Matangazo ya kibiashara

Afisa mmoja kutoka ujumbe wa Iran amesema ni budi mataifa hayo yapitie tena mapendekezo yao waliyotoa kwa kile alichodai kuwa hayana msingi wa kutosha kufanya kurudi tena kwenye mazungumzo baada ya mkutano wa Baghdad.

Vyombo vya habari vya Iran vimedai kuwa mapendekezo hayo yamepitwa na wakati, na yanaegemea upande mmoja.

Mapendekezo mapya yaliyotolewa na Mkuu wa Sera za mambo ya nje kutoka umoja wa Ulaya Catherine Ashton kwa niaba ya mataifa sita yenye nguvu duniani ni pamoja na Iran kupunguza mpango wake wa urutubishaji wa madini ya Uranium kwa asilimia 20.

Nchi hizo zimeahidi mambo mbalimbali ikiwemo kutoiwekea zaidi vikwazo nchi ya Iran, na kuondoa marufuku ya mafuta lakini nchi hizo hazikutaja matakwa ya Iran ya kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kulegeza vikwazo vilivyowekwa miaka ya karibuni.