SYRIA-UMOJA WA MATAIFA

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN lalaani vifo vya watu 108 nchini Syria huku Annan akizuru kujionea hali halisi

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN limeishukia na kuishutumu serikali ya Syria kwa kutumia makundi ya watu wenye silaha kutekeleza mauaji ya raia mia moja na nane na kuwajeruhi wengine zaidi ya mia tatu katika Kijiji cha Houla kilichopo karibu na Jiji la Homs na tayari Mpatanishi wa Kimataifa wa mgogoro wa nchi hiyo Kofi Annan anazuru Damascus kujionea hali halisi.

Watu waliopoteza maisha kwenye Kijiji cha Houla nchini Syria wakati watu wenye silaha walivyofanya shambulizi kwenye eneo hilo na kuua watu 108
Watu waliopoteza maisha kwenye Kijiji cha Houla nchini Syria wakati watu wenye silaha walivyofanya shambulizi kwenye eneo hilo na kuua watu 108 REUTERS/Shaam News Network/Handout
Matangazo ya kibiashara

Miongoni mwa waliopoteza maisha ni pamoja na watoto arobaini na tisa na wanawake thelathini na wanne ambao walikuwepo kwenye Kijiji cha Houla kipindi ambacho mauaji hayo mabaya zaidi yakitokea tangu kusitishwa kwa mapigano kutangazwe chini ya Mpatanishi Kofi Annan.

Taarifa ya Baraza la Usalama imesema kuwa vifo hivyo vimethibitishwa na waangalizi wa Umoja wa Mataifa UN na wamekiri hayo ni matokeo ya mashambulizi mfululizo ambayo yamekuwa yakipangwa na serikali dhidi ya wananchi wanaopinga serikali ya Rais Bashar Al Assad.

Urusi ambayo ni rafiki mkubwa kwa Syria imekuwa ni miongoni mwa mataifa kumi na tano wanachama wa Baraza la Usalama ambao wamesaini taarifa ya kulaani vifo ambavyo vimetokea katika Kijiji Cha Houla.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN limemtaka Rais Assad kuondoa mara moja wanajeshi wake na vifaru ambavyo vimeendelea kushuhudiwa katika makazi ya watu ili kutekeleza kwa vitendo mapendekezo ya Mpatanishi wa mgogoro huo Annan.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon na Mpatanishi Annan kila mmoja kwa wakati wake amesema mauaji hayo ni kitendo ambacho kimekwenda kinyume na sheria za kimataifa na hivyo hakitakiwi kujirudi wakati huu juhudi za kumaliza mauaji zikiendelea kuchukuliwa.

Iran nayo imelaani mauaji hayo na kusema ni shambulizi lililotekelezwa na magaidi na hivyo kuitaka serikali ya Syria kuwachukuliwa hatua kali wale wote ambao kwa namna moja wamehusika kwenye tukio hilo baya.

Ujerumani kupitia Balozi wake katika Umoja wa Mataifa UN Peter Witting amesema kumekuwa na ushahidi wa kutosha ambao unadhihirisha kumekuwa na matumizi ya silaha nzito pamoja na mizinga kitu ambacho ni hatari kwenye mgogoro unaoendelea.

Lakini serikali ya Syria yenyewe imekanusha vikali tuhuma za wao kuwaua wananchi wake ambapo Balozi wao katika Umoja wa Mataifa UN Bashar Jaafari amesema kamwe hawawezi kuthubutu kufanya kitendo kama hicho.

Kilio kikubwa kimekuwa ni kuendelea kutolewa kwa silaha kwa serikali na hata makundi mengine kitu ambacho kimelaaniwa na Jumuiya ya Kimataifa ambayo inataka kisitishwe mara moja ili kupata suluhuya mgogoro unaoendelea na kudumu kwa miezi kumi na minne sasa.