UINGEREZA

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Blair amehojiwa na Kamati Maalum ya Maadili ya Vyombo vya Habari na kukataa kuomba radhi

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair akihojiwa na Kamati Maalum ya Maadili ya Vyombo vya Habari
Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair akihojiwa na Kamati Maalum ya Maadili ya Vyombo vya Habari Reuters

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair amehojiwa na Kamati Maalumu ya Maadili ya Vyombo vya Habari nchini humo kuhusiana na ushiriki wake na wamiliki wa Kampuni ya News Of The World na amekataa kuomba radhi kwa chochote ambacho kilitokea wakati yeye yupo madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Blair alijitokeza hii leo asubuhi mbele ya Kamati hiyo kwa ajili ya kuhojiwa na kisha akaweka bayana uhusiano wake na Rupert Murdoch ulikuwa ni wa kikazi pekee hakuna mahusiano mengine nje ya kazi.

Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Uingereza Blair amesema alikuwa makini sana wakati wa utawala wake na ndiyo maana akaamua kutenganisha mahusiano yake binafsi na yake ya kikazi ili kutoa uhuru kwa Vyombo vya habari kufanyakazi zake.

Blair bila ya wasiwasi wowote huku akijiamini kupita kiasi ameiambia Kamati hiyo uhusiano wake na Mkurugenzi wa Kampuni ya New Corporation Murdoch ulijiegemeza kikazi tu na hawezi kuendesha mahusiano binafsi kwenye kazi.

Mahojiano hayo yaligubikwa na maandamano ya wananchi wenye hasira ambao wamekuwa mstari wa mbele wakimtuhumu Blair kufahamu kile ambacho kilitokea wakati yeye yupo madarakani na uchunguzi wa simu ambao ulifanya na Kampuni ya News Corporation.

Blair anatuhumiwa kuchukua hongo kutoka kwa Murdoch kitu ambacho mwenyewe amekipinga kwa nguvu zake zote na kukiri kitendo kama hicho hakipo bali ni tuhuma tu ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake.

Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Uingereza ameitaka Kamati hiyo kuhakikisha inafanyakazi zake kwa umakini bila ya kushinikizwa na upande wowote kitu ambacho kitasaidia kwa kiasi kikubwa kubaini ukweli wa jambo hili.