SYRIA

Koffi Annan kukutana na Rais Assad kujadili mustakabali wa baadaye wa Syria baada ya mauaji kuendelea

Mpatanishi wa Kimataifa wa Mgogoro wa Syria Kofi Annan anayetarajiwa kukutana na Rais Bashar Al Assad
Mpatanishi wa Kimataifa wa Mgogoro wa Syria Kofi Annan anayetarajiwa kukutana na Rais Bashar Al Assad Reuters

Mpatanishi wa Kimataifa kutoka Umoja wa Mataifa UN na Jumuiya ya nchi za Kiarabu kwenye mgogoro wa Syria Kofi Annan anatarajiwa kukutana na Rais Bashar Al Assad kwa ajili ya kuzungumzia namna ya kutekeleza mpango wa amani ambao ameupendekeza ili kumaliza umwagaji damu.

Matangazo ya kibiashara

Annan atakutana na Rais Assad siku mbili baada ya kushuhudiwa mauaji ya kinyama kwa raia mia moja na nane yaliyotekelezwa katika Kijiji cha Houla kilichopo katika Jiji la Homs na kusababisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN kutoa tamko kali kulaani kile kinachoendelea.

Mpatanishi huyo amesema lengo la mazungumzo yake na Rais Assad ni kubaini ukweli juu ya mustakabali wa baadaye wa Syria ambayo kila kukicha imeendelea kushuhudia mauaji ya raia wasio na hatia licha ya pande zinazokinzana kukubaliana kusitisha mauaji.

Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa UN Annan alipowasili Damascus hakusita kulaani mauaji hayo ambayo yalitokea mwishoni mwa juma na kusema kama yataendelea yatakwaza juhudi za kumaliza umwagaji wa damu ambao unazidi kuota mizizi.

Annan punde tu baada ya kuwasili huko Damascus akakutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid Al Muallem ambaye alimweleza kile ambacho alikiita ukweli juu ya mashambulia ambayo yamekuwa yakiendelea kushuhudiwa na kuchangia uharibifu mkubwa.

Mkutano huo wa Annan na Muallem ulihudhuriwa na Mkuu wa Waangalizi wa Umoja wa Mataifa UN waliopo nchini Syria kujionea hali halisi Meja Jenerali Robert Mood ambao kwa kauli moja wametaka mauaji yanayoendelea yasitishwe.

Annan hakusita kuendelea kusisitiza umuhimu wa kutekelezwa kwa mapendekezo sita ambayo aliyaainisha ikiwa ni sehemu ya kutaka kumaliza umwagaji wa damu ambao umedumu kwa karibu miezi kumi na mitano sasa.