MISRI

Waandamanaji Nchini Misri wachoma moto ofisi ya Mgombea wa Urais Ahmad Shafiq baada ya kutangazwa kwa matokeo

Waandamanaji nchini Misri wakiwa wamechoma moto Makao Makuu ya Mgombea wa Urais Ahmad Shafiq
Waandamanaji nchini Misri wakiwa wamechoma moto Makao Makuu ya Mgombea wa Urais Ahmad Shafiq

Waandamanaji wenye hasira nchini Misri wamechoma moto Makao Makuu ya Mgombea wa Urais na Waziri Mkuu wa zamani chini ya Utawala wa Rais Hosni Mubarak, Ahmad Shafiq muda mchache baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza matokeo yanayoonesha ameshika nafasi ya pili nyuma ya Mohammed Mursi.

Matangazo ya kibiashara

Wandamanaji hao walidhamia ofisi ya Shafiq na kuchoma moto kuonesha kukwera na hatua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kumtangaza yeye kama mshindi wa pili na hivyo analazimika kuingia kwenye duru la pili la uchaguzi dhidi ya Mursi ili kuamua nani atakuwa rais kumaliza utawala wa kijeshi chini ya Field Marsha Mohammed Hussein Tantawi.

Jeshi la Polisi limesema tayari limewakamata watuhumiwa wanane ambao wametajwa kuhusika kwenye mashambulizi hayo ambayo yamechangia kuchomwa moto kwa ofisi hizo za Shafiq.

Waandamanaji wengine baada ya kuteketeza kwa moto ofisi ya Shafiq wakarejea kwenye viunga vya Tahrir ambapo walirusha baadhi ya vipeperushi ambavyo walivichukua kutoka katika ofisi hizo.

Waandamanaji hao ambao wengi wanatajwa kutoka mrengo wa kuchoto hawawaungi mkono wagombea hao wawili ambao wamesalia kwenye duru la pili ili kuamua nani awe rais ajaye baada ya Mubarak.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Misri ilitangaza matokeo ya mwisho hiyo jana ambapo Mgombea kutoka Chama Cha Muslim Brotherhood Mursi alipata asilimi 24.77 ya kura zote na kufuatiwa na Shafiq aliyepata asilimia 23.66.

Hamdeen Sabbahi yeye ameambulia asilimia 20.71 akimshinda Abdel Moneim Abul Fotouh aliyepata asilimia 17.47 wakati nafasi ya tano ikichukuliwa na Amr Musa ambaye ameambulia asilimia 11.12 ya kura zote.

Mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi Faruq Sultan amesema wametupilia mbali mapingamizi saba ambayo yaliwasilishwa dhidi ya wagombea kati ya tarehe 26 na 27 kitu ambacho hakijaathiri matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo.

Duru la Pili la Uchaguzi wa Rais nchini Misri linatarajiwa kuwakutanisha Waziri Mkuu wa zamani Ahmad Shafiq dhidi ya Mgombea kutoka Chama Cha Muslim Brotherhood Mohammed Mursi.