SYRIA

Annan amwambia Rais Assad Syria inaelekea kubaya wakati Nchi za Magharibi zikiwatimua Mabalozi wa nchi hiyo

Mpatanishi wa Kimataifa kwenye mgogoro wa Syria Kofi Annan akiwa kwenye mazungumzo na Rais Bashar Al Assad
Mpatanishi wa Kimataifa kwenye mgogoro wa Syria Kofi Annan akiwa kwenye mazungumzo na Rais Bashar Al Assad REUTERS/SANA

Mpatanishi wa Kimataifa kutoka Umoja wa Mataifa UN na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwenye mgogoro wa Syria Kofi Annan amemsihi Rais Bashar Al Assada kutekeleza kwa vitendo utekelezaji wa umalizwaji wa umwagaji wa damua ambao umedumu kwa miezi kumi na tano sasa huku Mataifa ya Magharibi yakiamuru kuondoka kwa Mabalozi wa Damascus kwenye nchi zao.

Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo baina ya Annan na Rais Assada ambayo yamefanyika Damascus yametamatika kwa Viongozi hao kuafikiana kuendelea kuhakikisha umwagaji wa damu unamalizwa ili mchakato wa kisiasa uanze kuchukua nafasi yake na kumaliza hofu ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika taifa hilo.

Annan amemweleza Rais Assad kule ambako nchi yake inaelekea kubaya kutokana na kuendelea kushuhudiwa umwagaji wa damu ambao ulistahili kusitishwa ili kuruhusu mazungumzo baina ya pande zinazokinzana yachukue nafasi yake.

Rais Assad kwa upande wake amemjibu Annan kwa kumueleza mapendekezo hayo yatatekelezwa pale ambapo matukio ya kigaidi yatakapositishwa na wapinzani ambao wamekuwa wakipanga na kutekeleza mashambulizi kwenye Jiji la Damascus.

Mkutano huo ulikwenda sambamba na Nchi kumi na moja kuamuru Mabalozi wa Syria katika nchi hizo kuondaka mara moja ikiwa ni sehemu ya kuonesha kupinga mauaji ya watu mia moja na nane ambayo yalitokea katika eneo la Houla uliopo kwenye Jiji la Homs kitu ambacho kilizusha hasira kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Italia, Australia, Canada, Uhispania, Ubelgiji, Bulgaria na Uholanzindiyo nchi ambazo zimetangaza kuwaondoa Mabalozi wa Syria ambao wapo kwenye mataifa hayo wakisema hawaridhishwi na utekelezaji wa mapendekezo ya Annan kwenye kumaliza umwagaji wa damu.

Japan nayo imekuwa nchi nyingine ambayo imeungana na Mataifa hayo ya Magharibi kuamuru Balozi wa Syria huko Tokyo arudi nyumbani kutokana na kukerwa na jinsi serikali ya Rais Assad inavyoshughulikia kumaliza umwagaji wa damu uliodumu kwa miezi kumi na mitano sasa.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande yeye amesema dunia haifai kukaa kimya kwa kile ambacho kinaendelea kushuhudiwa nchini Syria chini ya Utawala wa Rais Assad akiituhumu serikali hiyo kuendelea kufanya mauaji ya kinyama dhidi ya raia wake.

Haya yanakuja huku Mashirika yasiyo ya Kiserikali yakisema watu tisini na wanane wameuawa siku ya jumanne wakati Rais Assad akiwa kwenye mazungumzo na Annan kuangalia namna ya kumaliza umwagaji damu.

Takwimu zinaonesha zaidi ya watu elfu kumi na tatu wameuawa tangu kuanza kwa machafuko ya kupinga utawala wa Rais Assad ambayo yalianza mwezi March mwaka jana na hadi sasa suluhu ya kudumu haijapatikana.