MYANMAR-THAILAND

Kiongozi wa Upinzani Nchini Myanmar Suu Kyi azuru Thailand na kuwaahidi wahamiaji atawasaidia kurejea nyumbani

Kiongozi wa Upinzani nchini Myanmar Aung San Suu Kyi akiwasili Uwanja wa Ndege wa Bangkok, Thailand
Kiongozi wa Upinzani nchini Myanmar Aung San Suu Kyi akiwasili Uwanja wa Ndege wa Bangkok, Thailand REUTERS/Soe Zeya Tun

Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini Myanmar na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Aung San Suu Kyi amewasili nchini Thailand ikiwa ni zaira yake ya kwanza kuifanya katika kipindi cha miaka ishirini baada ya kukabiliwa na kifungo cha ndani chini ya Utawala wa Kijeshi nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Suu Kyi amewasili nchini Thailand kuhudhuria mkutano wa kiuchumi ambao utazileta pamoja nchi za Ukanda wa Asia na kujiegemeza kutupia jicho hatua za kimaendeleo kwenye masuala ya biashara na uhusiano wa eneo hilo.

Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel amewasili Bangkok na kupata mapokezi ya kipekee kwa mamia ya watu waliojitokeza kumpokea huku wakimsifu kwa hatua ambazo amezipiga kwenye harakati zake za kurejesha demokrasia katika taifa hilo.

Suu Kyi mwenyewe amewaambia wafuasi wake waliojitokeza kumpoke huko Bangkok kwamba hawastahili kujiona kama wanyonge na watu wasio na nguvu na badala yake inabidi wapambane kwenye kila jambo ambalo wamepanga kulitekeleza.

Kiongozi huyo wa Chama NLD ambaye pia ni Mbunge aliwasili katika eneo ambalo linakaliwa na wahamiaji wengi katika Mji wa Mahachai ambapo wengi wa raia wa Myanmar wamemweleza wanataka kurejea nyumbani.

Suu Kyi bila ya kutafuna maneno aliwaambia raia hao wa Myanmar ambao wanaishi Thailand kuwa atafanya kila linalowezekana katika kuhakikisha wanarejea nyumbani baada ya kuishi uhamishono kwa muda mrefu.

Wahamiaji hao walikuwa na furaha iliyopita kifani kutokana na kumwona Kiongozi huyo wa Upinzani nchini Myanmar Suu Kyi ambaye amekumstari wa mbele kupigania uwepo wa demokrasia katika Taifa hilo.