LIBERIA-SIERRA LEONE-UHOLANZI

Mahakama Maalum ya Mauaji ya Sierra Leone SCSL yamfunga miaka 50 jela Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor

Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 50 kwa makosa ya uhalifu wa kivita aliyoyatenda nchini Sierra Leone
Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 50 kwa makosa ya uhalifu wa kivita aliyoyatenda nchini Sierra Leone REUTERS/Toussaint Kluiters/United Photos

Mahakama Maalum inayosikiliza Makosa ya Uhalifu nchini Sierra Leone SCSL iliyopo The Hague nchini Uholanzi imemhukumu kifungo cha miaka hamsini jela Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor ambaye alikutwa na hatia ya kutenda makosa kumi na moja ya uhalifu wa kivita nchini Sierra Leone.

Matangazo ya kibiashara

Mahakama Maalum inayosikiliza Makosa ya Uhalifu nchini Sierra Leone SCSL ilimkuta na hatia ya kutenda makosa kumi na moja Taylor mwezi April mwaka huu kutokana na kufadhili Waasi ambao waliendesha mauaji katika nchi ya Liberia ambao wanatambulika kama RUF ambao walikuwa wanabadilishana silaha kwa almasi.

Jaji Richard Lussick ambaye alikuwa anasikiliza kesi hiyo dhidi ya Taylor ambaye ametenda makosa hayo kati ya mwaka elfu moja mia kenda tisini na moja hadi elfu mbili na moja amemhukumu kifungo cha miaka hamsini jela ambapo atafungwa nchini Uingereza.

Hukumu hii ya miaka hamsini dhidi ya Taylor inakuwa ni pungufu kwa miaka thelathini ukilinganisha na kifungo ambacho alipendekeza Mwendesha Mashtaka Brenda Hollis ambaye alitaka Rais huyo wa zamani wa Liberia ahukumiwe kifungo cha miaka themanini jela.

Jaji Lussick ambaye alikuwa anaongoza jopo la majaji alianza kwa kusoma mashtaka yote ambayo yanamkabili Taylor aliyotenda akiwa Rais wa Liberia katika nchi jirani ya Sierra Leone ambapo alifadhili pakubwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hukumu hiyo inakuwa ya kwanza kutokelewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC tangu imeanza kazi zake na Taylor anakuwa Kiongozi wa kwanza wa nchi kukumbana na kifungo mbele ya Mahakama hiyo yenye maskani yake huko The Hague.

Taylor alikutwa na makosa kumi na moja tarehe ishirini na sita ya mwezi April baada ya ushahidi kudhihirisha alilifadhili Kundi la Waasi la RUF ambalo liliendesha vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyosababisha vifo vya watu laki moja na elfu ishirini.

Taylor alikuwa akitoa silaha kwa Kundi la Waasi la RUF ambalo lenyewe lilikuwa likimpatia almasi huku Kundi hilo likiendelea kutekeleza ubakaji na mauaji sambamba na kuajiri watoto wenye chini ya umri wa miaka kumi na tano kwenye jeshi lao.

Taylor kwenye ushahidi wake ambao aliotoa kwenye Mahakama ya SCSL alisema kuwa hongo ilitumika kwa mashahidi ili waweze kutoa ushahidi wa uongo dhidi yake na ukweli ni kwamba yeye hajahusika na kufadhili vita hivyo.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone vilizuka mwaka 1991 na kutamatika mwaka 2001 ambapo watu wengi wameathiriwa kwa kubakia na ulemavu wa maisha sambamba na wengine 120,000 kupoteza maisha.