MAREKANI

Mitt Romney akaribia kupata nafasi ya kuwa Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama Cha Republican

Mitt Romney akiwa kwenye kampeni za kusaka kuwa mgombea wa urais kupitia tiketi ya Chama Cha Republican
Mitt Romney akiwa kwenye kampeni za kusaka kuwa mgombea wa urais kupitia tiketi ya Chama Cha Republican REUTERS/Darren Hauck

Mchakato wa kupata mgombea wa urais kupitia Chama Cha Republican nchini Marekani unaonekana kufikia patamu huku kila dalili zikionesha Mitt Romney ndiyo mwenye nafasi ya kupeperusha bendera ya Chama hicho kwenye uchaguzi wa Urais baadaye mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Njia imezidi kuwa nyeupe kwa Romney baada ya kufanikiwa kwenye kura za maoni katika Jimbo la Texas kitu ambacho kimedhihirisha anaendelea kuungwa mkono na wanachama wengi wa Chama Cha Republican ikilinganisha na wagombea wengine.

Romney amejisafishia njia na amejiwekea mazingira mazuri ya kuwa mshindani wa Rais wa sasa wa Marekani Barack Obama ambaye atakiwakilisha Chama Cha Democratic kwenye kinyang'anyiro cha urais mnamo mwezi Novemba mwaka huu.

Kabla ya kuidhinishwa kuwa mgombea rasmi wa Chama Cha Republican kwenye mkutano mkuu wa Chama hicho Romney anatakiwa aungwe mkono na wajumbe elfu moja mia moja na arobaini na nne ndiyo apate ridhaa ya kuwa mgombea.

Romney anaonekana kuwazidi wagombea wengine ambao walikuwa wanasaka ridhaa ya Chama cha Republican kupeperusha bendera yao na mkutano wa mwisho utafanyika katika Jimbo la Florida mnamo mwezi August.

Kabla hajaingia kwenye kura za maoni kwenye Jimbo la Texas Romney alikuwa na wajumbe elfu moja na themanini na sita na hivyo anahitaji wajumbe hamsini na nane pekee ili afikie idadi inayotakiwa ya kuungwa mkono na wajumbe elfu moja mia moja na arobaini na wanne.

Nafasi ya Romney ilizidi kuwa kubwa baada ya baadhi ya wagombea kujiondoa kwenye mbio za kusaka kuteuliwa kuwa mgombea kupitia tiketi ya Chama Cha Republican kwenye uchaguzi wa baadaye mwaka huu.

Mkutano mkuu wa Chama Cha Republican Jimboni Florida ndiyo utakuwa wa mwisho kwa ajili ya kuidhinisha yule ambaye atapambana na Rais Barack Obama kwenye uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka huu.