SOMALIA-UTURUKI

Ban atoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete ili kuzuia ombwe la Uongozi nchini Somalia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon akiwa na Rais wa Somalia Sharif Sheikh Ahmed wakiwa kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Istanbul huko Uturuki
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon akiwa na Rais wa Somalia Sharif Sheikh Ahmed wakiwa kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Istanbul huko Uturuki

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa msaada wa haraka kwa nchi ya Somalia ili iweze kujijenga upya na kuepukana na ombwe la uongozi wakati huu ambapo serikali ya mpito muda wake unaelekea ukingoni.

Matangazo ya kibiashara

Ban akihutubia Mkutano wa Kimataifa juu ya kuangalia hatima ya baadaye ya Somalia ambao unafanyika nchini Uturuki amesema Dunia inatakiwa iungane kutoa msaada wa haraka katika kukabiliana na kitisho cha kushuhudia ombwe la uongozi katika nchi hiyo iliyo kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Katibu Mkuu wa UN ametoa ushauri kwa nchi wahisani kuchangia kwenye juhudi ambazo zinafanyika katika kuisaidia Somalia ijijenga upya na kushiriki ipasavyo kwenye vita ya kupambana na ugaidi, uharamia na ukame ambao umekuwa chanzo cha uwepo wa njaa kwenye taifa hilo la Pembe ya Afrika.

Ban amewaambia wajumbe zaidi ya hasmini kutoka nchi ambazo zinashiriki kwenye Mkutano huo wa Kimataifa nchini Uturuki ya kwamba kila nchi inastahili kuchukua hatua kwa yale ambayo yanashuhudiwa nchini Somalia ili kuweza kuyapatia suluhu ya kudumu.

Kauli ya Ban imeendelea kuzilenga nchi ambazo zinauwezo wa kusaidia kupatikana kwa utulivu nchini Somalia zifanye hivyo kwani hiyo itasaidia kuifanya nchi hiyo iwe sehemu salama kwa wananchi na hawa wageni ambao wamekuwa wakifanya safari kuelekea huko.

Wenyeji wa Mkutano huo ni Uturuki ambapo kupitia Waziri wa Mambo ya Nje Ahmet Davutoglu amesema Somalia inahitaji msaada zaidi kutoka kwa mataifa mbalimbali ambayo yamekuwa karibu kuisaidia.

Mkutano huu wa siku mbili unatarajiwa kutamatika hii leo baada ya kuanza hiyo jana kujadili miaka zaidi ya ishirini ya machafuko ambayo yamekuwa yakitokea nchini Somalia na kusababisha vifo vya watu zaidi ya laki nne.

Serikali ya mpito chini ya Rais Sharif Sheikh Ahmed imekuwa kwenye wakati mgumu kutokana na upinzani mkali inaoupata kutoka kwa Kundi la Wanamgambo wa Al Shababa lenye utawala kwenye maeneo mengi ya nchi hiyo.