MYANMAR-THAILAND

Suu Kyi aomba wawekezaji wasaidie kuimarisha uchumi wa Myanmar na kuondoa tatizo la ajira

Kiongozi wa Upinzani Nchini Myanmar Aung San Suu Kyi akihutubia Mkutano wa Uchumi kwa Mataifa ya Asia huko Thailand
Kiongozi wa Upinzani Nchini Myanmar Aung San Suu Kyi akihutubia Mkutano wa Uchumi kwa Mataifa ya Asia huko Thailand

Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini Myanmar na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Aung San Suu Kyi ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kujitokeza na kuwekeza katika nchi hiyo ambayo inaendelea kutekeleza mabadiliko ya siasa baada ya kuondoka chini ya makucha ya utawala wa Kijeshi.

Matangazo ya kibiashara

Suu Kyi ametoa wito huo kwenye Mkutano wa Kiuchumi wa Mataifa ya Asia na kuzitaka nchi zenye utajiri wa viwanda kueleka nchini Myanmar kuwekeza ili kusaidia kukua kwa uchumi huo kitu ambacho kitasaidia kuleta maendeleo kwa wananchi wa taifa hilo ambao walikuwa kwenye mbinyo mkubwa wa kisiasa.

Kiongozi huyo Mkuu wa Upinzani kutoka Chama Cha NLD nchini Myanmar amesema kilio kikubwa cha wananchi wa taifa lao ni ukosefu wa ajira ambapo vijana wengi wameshindwa kupata kazi kutokana na kutokuwepo kwa shughuli za kutosha za uwekezaji na uzalishaji.

Suu Kyi amesema huu ni wakati muafaka kwa wawekezaji kutumia fursa hii ili kuijenga upya Myanmar ambayo inahitaji msaada mkubwa kutoka mataifa yenye uchumi imara ili iweze kupiga hatua za haraka baada ya kukabiliwa na vikwazo vya kiuchumi kwa muda mrefu.

Licha ya kutoa wito kwa wawekezaji kueleka nchini Myanmar Suu Kyi amesema nchi yake inasheria nzuri lakini tatizo jingine ambalo lipo ni mfumo wa kimahakama na hivyo wanahitaji uwepo wa msukumo wa kimataifa kwenye kutekeleza mabadiliko hayo muhimu.

Suu Kyi amesema hilo linatakiwa lifanywe pia na serikali ya nchi yake kitu ambacho kitasaidia wawekezaji kuwa huru na kujitokeza kwenda kuwekeza na kuharakisha maendeleo ambayo yamekuwa kwenye ndoto za wananchi wa taifa hilo kwa miaka nenda rudi.

Makampuni mengi yalishikwa na hasira na hivyo kujiondoa kwenye uwekezaji nchini Myanmar punde tu baada ya Jumuiya ya Kimataifa kutumia rungu lake na kuweka vikwazo kutokana na nchi hiyo kupuuza uwepo wa demokrasia.

Hii ni zara ya kwanza ya nje ya nchi kufanywa na Aung San Suu Kyi ambaye kwa kipindi cha miaka ishirini na minne alikuwa kwenye kifungo cha ndani wakati nchi hiyo ikiongozwa na Utawala wa Kijeshi.