SYRIA

Syria yawalaumu Waasi kutekeleza mauaji huko Houla huku Urusi ikilaumiwa kwa kuiuzia silaha Damascus

Miili ya watu waliouawa katika eneo la Houla ambao serikali imesema uchunguzi umebaini waliuawa na Waasi
Miili ya watu waliouawa katika eneo la Houla ambao serikali imesema uchunguzi umebaini waliuawa na Waasi

Mataifa ya Magharibi yameendelea kuituhumu Urusi kutokana na kuendelea kuiuzia silaha serikali ya Syria wakiona hatua hiyo inaweza kuongeza mauaji katika nchi hiyo iliyo kwenye machafuko yaliyodumu kwa miezi kumi na tano sasa huku serikali ikilaumu waasi kwa kuendeleza mauaji ya kinyama.

Matangazo ya kibiashara

Marekani imekuwa mstari wa mbele kuishutumu Urusi kwa kuendelea kufanya biashara ya silaha na Syria kitu ambacho kitakwamisha juhudi za Mpatanishi wa Umoja wa Mataifa UN na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Kofi Annan za kutaka kumaliza umwagaji wa damu unaoendelea kushuhudiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton akiwa ziarani nchini Denmark amesema wakati umefika kwa Urusi kuunga mkono mapendekezo ya Umoja wa Mataifa UN yanayotolewa dhidi ya Utawala wa Rais Bashar Al Assad ili kunusuru vifo zaidi ambavyo vinaweza kujitokeza.

Madai haya yanatolewa wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN likijiandaa kukutana na kujadili hali ya kibinadamu katika nchi hiyo kutokana na kuendelea kuwepo kwa taarifa za kuibuka kwa vifo kila uchao katika maeneo mbalimbali nchini humo licha ya uwepo wa Waangalizi wa Umoja huo.

Nayo serikali ya Syria imesema kwenye uchunguzi wake ilioufanya juu ya mauaji ya kinyama yaliyofanyika katika eneo la Houla lililopo katika Jiji la Homs wamebaini waasi ndiyo ambao walitekeleza mauaji hayo ya raia zaidi wa mia moja na nane.

Mkuu wa Uchunguzi wa Serikali Jenerali Qassem Jamal Suleiman amesema wamebaini watu ambao wameuawa kwenye eneo la Houla ni wale ambao walikuwa wanapinga uwepo wa waasi na kuendelea kuunga mkono serikali ambayo ipo madarakani.

Maelezo hayo ya Tume ya Uchunguzi nchini Syria yamepingwa vikali na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN ambalo limesema maelezo hayo ya serikali ni ya uongo na imekuwa ikijitetea kwa mauaji ambayo inayafanya yenyewe.

Balozi wa Marekani katika Baraza la Usalama Susan Rice amesema serikali imeshindwa kutoa vithibitisho sahihi vya kudhihirisha kama kweli serikali haikuhisika na mauaji hayo ambayo yalitokea huko Houla.

Kwa upande wake serikali ya Uingereza kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje William Hague amesema kile ambacho kinashuhudiwa nchini Syria hakifai kuendelea kwani kinaleta madhara zaidi.