NIGERIA

Siku tatu za maombolezi zatangazwa nchini Nigeria kutokana na ajali ya ndege.

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ametangaza siku tatu ya kitaifa ya maombolezo kutokana na vifo vya abiria 153 vilivyotokea baada ya ndege yao kuanguka mjini Lagos siku ya Jumapili.

Matangazo ya kibiashara

Rais Jonathan pia ametaka uchunguzi kufanyika haraka iwezekanavyo kubaini chanzo cha ajali hiyo ya ndege iliyoangukia majengo katika mji huo wa Lagos wenye idadi kubwa ya watu.

Inaelezwa ndege hiyo ya abiria aina ya Dana inayomilikiwa na kampuni ya India, iligonga majengo kabla ya kuanguka na kuwaka moto huku ikiaminika kuwa ajali hiyo pia imesababisha idadi kubwa ya watu kuuawa baada ya majengo waliyokuwemo kuangukia na ndege hiyo.

Ripoti ya awali inaonesha kuwa bado kiini cha ajali hiyo haijafamika lakini maafisa wa uokozi wanasema kifaa cha kunasa sauti kimepatikana na kukabidhiwa polisi,kwa uchunguzi zaidi.

Mapema mwezi uliopita ndege nyingine ya kampuni ya Dana ilikumbwa na hitilafu ya kimitambo na kulazimika kutua mjini Lagos muda mfupi tu baada ya kupaa angani.

Nigeria kama mataifa mengine barani Afrika bado inakumbwa na ukosefu wa usalama wa angaa,huku serikali ya Nigeria mwaka 2005 ikifanya jitihada za kuimarisha usalama katika safari zake za angaani.

Idadi kubwa ya wasafari hutumia usafiri wa angaa kutoka uwanja wa kimataifa wa Murtala Mohammed mjini Lagos,kwenda katika mataifa mbalimbali katika mataifa ya Afrika Magharibi.