Uchina-Urusi

Vladimir Putin ziarani nchini Uchina kujadili machafuko nchini Syria

Rais wa Urusi Vladimir Putin amewasili nchini Uchina kwa ziara ya siku tatu, ziara ambayo rais huyo na mwenyeji wake Hu Jintao watazungumzia uhusiano wa mataifa hayo mawili pamoja na ule wa  kibiashara.

Matangazo ya kibiashara

Sera ya mataifa hayo mawili kuhusu machafuko yanayoendelea nchini Syria pia ni suala ambalo linatarajiwa kupewa kipau mbele katika mkutano wa viongozi hao wawili.

Urusi na Uchina wamekuwa na sera moja kuhusu machafuko yanayoendelea nchini Syria na wametumia kura zao za turufu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuzuia kupitishwa kwa azimio lolote dhidi ya serikali ya rais Bashar Al Assad.

Marekani na mataifa mengine ya Ulaya kwa upande wao wameendelea kuilaumu Moscow na Beijing kuhusu msimamo wao kuhusu namna ya kutatua machafuko yanayoendelea nchini ,sera ambayo Washington DC inasema inachangia kuongezeka kwa machafuko nchini Syria na huenda kukatokea kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Siku ya Jumatatu,viongozi wa Umoja wa Ulaya walikutana na rais Putin na kumtaka kuuungana na mataifa mengine ya Ulaya kumaliza machafuko yanayoendelea Syria kwa kuhakikisha kuwa mpango wa amani uliopendekezwa na msuluhishi wa kimataifa wa mgogoro huo Koffi Annan unazingatiwa.

Wakati hayo yakijiri, majeshi ya serikali ya Syria yamepambana na wapiganaji wa upinzani na kusabisha kuuawa kwa wanajeshi wa serikali 80 katika jijini Damascus na Idlib,kwa mujibu wa masharika ya kutetea haki za binadamu nchini humo.