Israel-Palestina

Isreal kuendelea kujenga makaazi mapya katika ukingo wa Magharibi

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametangaza kuwa serikali yake itajenga mamia ya makaazi ya walowezi katika ukingo wa Magharibi.

Matangazo ya kibiashara

Tangazo la Netanyahu linakuja siku moja baada ya bunge la Israel kupitisha mswada wa kutaka serikali kutoendelea kujenga maakazi kwa sababu ya kisheria.

Netanyahu ameongeza kuwa serikali yake haitaruhusu tofauti za kisheria kuathiri ujenzi wa makaazi mapya 300 katika ukingo huo wa Magharibi karibu na mji wa Ramallah katika ngome ya Palestina.

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amekashifu uamuzi wa Netanyahu na kusema kuwa ujenzi wa makaazi hayo mapya ,kutadhoofisha juhudi za kusaka amani kati yao na Israel.

Washington pia kupitia kwa msemaji wake wa wizara ya mambo ya nje Mark Tonner nayo imekashifu hatu hiyo ya Israel ikiongeza kuwa, Jerusalem inarudisha nyuma juhudi za kupata amani kati ya Waisraeli na Wapalestina.

Mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina yalivunjika miaka mitatu iliyopita na Palestina imesema kuwa haijarejea katika meza ya mazungumzo hadi pale Israel itakapoacha kujenga makaazi mapya katika ukingo wa Magharibi na Mashariki mwa mji wa Jerusalem.

Israel inasema mazungumzo hayo yanastahili kurejelewa bila ya masharti yeyote, wakati Palestina ikiendelea kuishtumu Israel kunyakua ardhi yao mwaka 1967.