Marekani-Somalia

Marekani yatoa Dola Milioni 33 kwa yeyote atakayetoa maelezo kuhusu viongozi wa Al-Shabab

Marekani imetoa Dola Milioni 33 kama zawadi kwa yeyote atakayetoa habari muhimu kuhusu viongozi wakuu wa wanagambo wa kigaidi wa Al-Shabab nchini Somalia.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mara ya kwanza Marekani imeorodhesha majina ya viongozi wa Al-Shabab inayowatafuta zaidi akiwemo mwanzilishi wa kundi hilo Ahmed Abdi aw-Mohamed.

Dola Milioni 7 zimetengwa kwa yeyote atakayetoa maelezo alikojificha Aw Mohamed ambaye sasa anatafutwa na Marekani kwa kutishia usalama wa Washington DC na mataifa mengine duniani hasa ya Afrika Mashariki na Kati.

Viongozi wengine wa Al-Shabab wanaotafutwa ni pamoja na Ibrahim Haji Jama, Fuad Mohamed Khalaf, Bashir Mohamed Mahamoud na Mukhtar Robow.

Tangu mwaka 2006 kundi la Al-Shabab limekuwa likitekeleza mashambulzi kadhaa ya bomu hasa mjini Mogadishu,Kampala Uganda na Nairobi nchini Kenya na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.

Kundi hili bado linathibiti Kusini kwa Somalia lakini wanajeshi wa Umoja wa Afrika, wanaojumuisha wale kutoka Ethiopia na Kenya wamefaulu kuchua tena uthibiti wa miji hiyo huku wanajeshi kutoka Uganda na Burundi wakithibiti mji mkuu Mogadishu.

Aidha,majeshi ya Kenya yamefaulu kuthibiti wa mji wa Afmado na sasa wanalenga kuchukua uthibiti wa mji wa Kismayu ambao ndio ngome kubwa ya Al-Shabab.

Serikali ya mpito nchini Somalia inatarajiwa kumaliza muda wake tarehe 20 mwezi Agosti mwaka huu na hivyo uchaguzi mkuu unatarajiwa kuandaliwa kuchagua serikali mpya.

Hali ya usalama nchini Somalia imedorora tangu mwaka 1991 wakati utawala wa rais wa zamani Mohamed Siad Barre ulipomalizika.