Syria

Marekani yaonya kuhusu njama mpya za serikali ya Syria kutekeleza mauaji

Picha inayoonyesha jiji la homs baada ya mashambulzi ya bomu Juni  11
Picha inayoonyesha jiji la homs baada ya mashambulzi ya bomu Juni 11 AFP PHOTO/YOUTUBE

Marekani inaonya kuwa serikali ya Syria inapanga mauaji mapya dhidi ya raia wake katika mji wa Haffa mkoani Latakia baada ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa kuzuiliwa kuingia katika mji huo. Jeshi la Syria linatumia mbinu mpya kwa kuwashambulia wananchi kwa ndege aina ya Helicopta.

Matangazo ya kibiashara

Ndege za kivita za serikali ya Syria zimeonekana zikifanya mashambulizi katika ngome za upinzani na kusababisha kuuawa kwa zaidi ya watu 100 kulingana na mashirika ya haki za binadamu nchini humo.

Ahmad Fawzi msemaji wa msuluhishi wa kimataifa wa mgogoro huo Koffi Annan amesema, Annan amesikitishwa na kuogopeshwa na mashambulizi yanayoendelea katika mji wa Homs, pia Annan anatiwa hofu na matumizi ya silaha nzito, Helicopta na mizinga huko Latakeya.

Victoria Nuland naye ni msemaji wa mambo ya nje wa Marekani amesema kwamba majeshi ya Syria yamedhohofisha hali ya amani nchini Syria kutokana na machafuko yanayotekelezwa na majeshi hayo hasa kwa kutumia mbinu mpya katika kushambulia raia, ikiwa ni pamoja na kutumia helicopta.

Victoria Nuland amewataka wanajeshi wa Syria kujifunza kile kilichotokea nchini Bosnia, huku akisema kwamba Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kuendelea kuwafumbia macho wanaotekeleza vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu.

Wakati hayo yakijiri ripoti ya Umoja wa Mataifa unasema kuwa watoto wanatumiwa kama ngao na majeshi ya serikali na wamekuwa wakilazimishwa kupanda katika magari ya kijeshi ili kuwakinga wanajeshi wa serikali.