TANZANIA-KENYA

Polisi ya Tanzania yamkamata mshukiwa wa mlipuko wa bomu mwezi uliopita nchini Kenya

Mshukiwa wa ulipuaji ma bomu nchini Kenya Emrah Erdogan
Mshukiwa wa ulipuaji ma bomu nchini Kenya Emrah Erdogan

Mtu mmoja anayeshukiwa kuwa ana uhusiano na shambulio la mwezi uliopita katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi amekamatwa nchini Tanzania. Akiongea na RFI Kiswahili kutoka jijini Dar Es Salaam Tanzania Msemaji wa polisi ya Tanzania Isaya Mngulu amesema kwamba  mtu huyo alikamatwa akiwa katika hoteli mojawapo jijini Dar Es Salaam na tayari wamewasiliana na viongozi wa Kenya na Uganda.

Matangazo ya kibiashara

Polisi ya Tanzania imethibitisha kuwa mtu huyo ajulikanae kwa jina la Emrah Erdogan ni raia wa Ujerumani mwenye asili ya Uturuki. Kenya inadai kuwa alivuka mpaka mapema mwezi Mayi kutoka Somalia ambako alishiriki mapigano kwa niaba ya kundi la Al Shabab.

Watu zaidi ya 30 walijeruhiwa katika mlipuko ambao polisi ya Kenya wanasema ulisababishwa na bomu hilo lililotegwa na mtu huyo.

Hata hivyo awali kulikuwepo na hali ya sintofahamu juu ya chanzo cha mlipuko huo- ambapo Maofisa wa Polisi walianza kwa kusema kuwa mlipuko huo ulisababishwa na hitilafu ya umeme.

Kundi la Al Shabab limeendeleza vitisho vya kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi nchini Kenya kwa sababu nchi hio ilituma vikosi nchini Somalia. Serikali ya Kenya inalituhumu kundi la wapiganaji wa Al Shabab kuhusiana na utekaji nyara wa watu kadhaa kwenye ardhi yake pamoja na kusababisha hali ya wasiwasi kwenye mpaka baina yake na Somalia.

Hali hii ndio ambayo iliopelekea vikosi vya Kenya kuingia nchini Somalia na kuanzisha operesheni Linda Nchi kabla ya kujiunga baadae na vikosi vya Umoja wa Afrika vilivyoko nchini Somalia AMISOM.

Mshukiwa huyo ni miongoni mwa watu wanne ambao Polisi ya Kenya imekua ikiwasaka tangu kutokea kwa mlipuko huo. Ilisambaza picha yake na kuomba habari kuhusu mahali alipo.