Syria

Hali yaendelea kuwa mbaya zaidi nchini Syria, wakati wanaharakati wakiitisha maandamano baada ya sala ya Ijumaa

Mashambulizi
Mashambulizi REUTERS/Shaam News Network/Handout

Maandamano ya umwagaji damu yanaendelea nchini Syria, ijumaa hii yakiwa yanaingia katika mwezi wa 16. waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius ametangaza uwezekano wa kufanyika mkutano wa kimataifa kuhusu Syria unaotarajiwa kufanyika Juni 30 Jijini Giniva nchini Uswisi bila hata hivyo kubainisha iwapo ndio ule mkutano uliotajwa na msuluhushi wa Kimataifa Kofi Annan. 

Matangazo ya kibiashara

Laurent Fabius amefahamisha pia kuwa mazungumzo yanaendelea kufanyika na urusi mshirika wa karibu wa serikali ya Syria kuhusu hatma ya Syria baada ya Bashar Al Assad.

Kama inavyo shuhudiwa tangu mwanzoni mwa maandamano machi 15 mwaka 2011, waandamanaji wanakusanyika baada ya sala ya Ijumaa na kuandamana huku wakitowa kauli za kuukashifu utawala wa rais Assad.

Hapo jana watu zaidi ya hamsini waliuliwa na wengine zaidi ishirini wamejeruhiwa katika matukio tofauti.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema zaidi ya watu elfu 14 wameuawa nchini Syria, idadi ambayo inatarajiwa kuongezeka ikiwa suluhu halitapatikana.

Marekani imeendelea kuishtumu Urusi kuwa kikwazo cha kumalizika kwa vita nchini Syria, huku Urusi nayo ikiilamu Marekani kwa kuwapa wapiganaji silaha.

Waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria wanasema kinachoendelea nchini humo ni vita vya wenyewe kwa wenyewe na hali ni mbaya katika maeneo mengi nchini humo.