CAIRO-MISRI

Chama cha Muslim Brotherhood chajitangazia ushindi kwenye uchaguzi wa Urais uliofanyika mwishoni mwa juma

Raia wa Misri akibusu picha ya mgombea urais wa chama cha Muslim Brotherhood Mohammed Mursi
Raia wa Misri akibusu picha ya mgombea urais wa chama cha Muslim Brotherhood Mohammed Mursi Reuters

Chama cha kiislamu cha Muslim Brotherhood nchini Misri kimejitangazia kushinda uchaguzi mkuu wa urais uliofanyika mwishoni mwa juma kwenye uchaguzi wa duru ya pili uliokuwa umegubikwa na mizozo. 

Matangazo ya kibiashara

Kundi la wanachama wa Muslim Brotherhood waliitisha mkutano na waandishi wa habari na kisha kumtangaza mgombea wao Mohammed Morsi kama mshindi wa uchaguzi huo kwa kupata kura milioni 12 sawa na asilimia 52.

Wanachama hao wameongeza kuwa mgombea wa upinzani Ahmed Shafiq amepata kura milioni 11.84 na hivyo chama chao kimeibuka na ushindi.

Morsi mwenye pia amezungumza kwenye mkutano huo na kuahidi kuleta mabadiliko makubwa nchini humo ikiwemo kuwaunganisha waumini wa makanisa ya Coptic na kwamba kila raia wa misri aliyeshiriki mapinduzi atakuwa kwenye familia yake.

Hata hivyo wakati wanachama hao wakijitangazia ushindi kwenye uchaguzi huo wa duru la pili tume ya taifa ya uchaguzi bado haijatangaza matokeo rasmi japo wachamabuzi wa mambo wanadai kuwa huenda yakabadilika.

Maelfu ya wananchi na wafuasi wa Muslim Brotherhood walisikika kwenye viunga vya mji wa Cairo wakilaani utawala wa kijeshi wakishinikiza utawala huo kuachia madaraka kwa serikali ya kiraia ambayo wamedai hakuna shaka chama chao kimeshinda.

Uchaguzi huo umefanyika wakati ambapo makataa ya kutotembea nyakati za usiku yamerejeshwa tena uamuzi abao wananchi waliandamana juma lililopita kupinga baraza la kijeshi kupewa mamlaka zaidi na mahakama.

Mbali na kurejeshwa kwa makataa hayo, mahakama ya katiba nchini humo juma lililopita pia ilitangaza kutolitambua bunge la nchi hiyo ikisema kuwa halikuwa halali na matokeo mengi ya uchaguzi wa wabunge hayakuwa sahihi na kwamba chama cha Muslim Brotherhood hakina mamlaka kwenye bunge la nchi hiyo.