ATHENS-UGIRIKI

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wapongeza ushindi wa chama cha New Democracy

Antonis Samaras,kiongozi wa chama cha New Democracy
Antonis Samaras,kiongozi wa chama cha New Democracy REUTERS/Panayiotis Tzamaros

Viongozi wa dunia wamepongeza ushindi mdogo wa chama cha New Democracy cha nchini Ugiriki kwenye uchaguzi wa ubunge uliofanyika mwishoni mwa juma na kutaka uundwaji wa haraka wa serikali ya umoja. 

Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Marekani kupitia taarifa iliyotolewa na ikulu ya nchi hiyo, imepongeza ushindi wa chama hicho na kuongeza kuwa ilikuwa ni matarajio ya viongozi wengi walioko kwenye Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kutaka kuona nchi hoyo inasalia kwenye ukanda wa Euro.

Hii leo viongozi wa nchi wanachama wa EU wanatarajiwa kukutana mjini Brussels Ubelgiji kwenye mkutano wa dharura kujadili kile kilichotokea nchini Ugiriki ikiwemo kuweka mikakati ya kukishauri chama hicho kukubali kuunda serikali ya Umoja na chama kinachounga mkono ubanaji matumizi.

Wakati asilimia 99 ya kura zikiwa zimekwishahesabiwa, wizara ya mambo ya ndani nchini humo imetangaza matokeo ambayo yanaonesha chama cha New Democracy kupata ushindi wa asilimia 29.7 na kupata viti 129, huku chama cha Syriza kikipata asilimia 26.9 na kupata viti 71 wakati chama cha Pasok kikipata asilimia 12.3 kwa kupata viti 33.

Chama cha New Democracy ambacho kilikuwa kwenye serikali ya umoja iliyovunjika kimekuwa mstari wa mbele kuunga mkono hatua za kubana matumizi ambazo chama cha Syriza kilichoibuka mshindi wa pili kimekuwa kikipinga sera hiyo.

Kiongozi wa chama cha New Democracy Antonis Samaras amesema kuwa ushindi wa chama chake umedhihirisha maamuzi ya wananchi wa Ugiriki ambao dhahiri wameonesha nia kutaka nchi yao kusalia kwenye Umoja wa Ulaya EU.

Hata hivyo chama cha Syriza kinachoongozwa na Alexis Tsipras ambacho kimekuwa mstari wa mbele kupinga hatua ya kubana matumizi, kiongozi wake amesema kuwa hatashirikiana na Serikali wala kushiriki kwenye mazungumzo ya uundaji wa Serikali ya Umoja.

Uamuzi wa chama hicho huenda ukachelewesha zaidi mchakato wa kupatikana kwa serikali ya Umoja ambapo chama cha New Democracy kitahitajika kukishawishi chama cha Pasok na Syriza kuunda serikali ya Umoja.