ATHENS-UGIRIKI

Hali bado haitabiriki kuhusu uundwaji wa Serikali ya muungano nchini Ugiriki

Kiongozi wa chama cha Syriza, Alexis Tsipras (kushoto) akizungumza na kiongozi wa chama chaNew Democracy, Antonis Samarás (kushoto)
Kiongozi wa chama cha Syriza, Alexis Tsipras (kushoto) akizungumza na kiongozi wa chama chaNew Democracy, Antonis Samarás (kushoto) Reuters

Chama kilichoshinda uchaguzi wa ubunge nchini Ugiriki cha New Democracy kinaendelea na mazungumzo na viongozi wa vyama vya upinzani nchini humo kuangalia uwezekano wa uundwaji wa serikali ya muungano.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa chama hicho Antonis Samaras amefanya mazungumzo na viongozi wa chama cha Pasok ambacho kiliibuka mshindi wa tatu kwenye uchaguzi kwenye mazungumzo yaliyoingia siku ya pili hii leo huku kukiwa bado hakuna muafaka.

Mara baada ya mazungumzo yake na viongozi wa chama cha Pasok, viongozi wa Pasok wenyewe hawakuwa tayari kusema kuwa wamekubaliana na mapendekezo ya chama cha New democracy katika uundwaji wa serikali ya muungano na kusema itatoa tamko lake baadae.

Chama cha New Democracy kimekuwa pia na mazungumzo na vyama vingine vidogo nchini humo ambavyo vinaonekana kuunga mkono hatua ya ubanaji matumizi inayopingwa na chama cha Syriza.

Chama cha Syria na muungano wa vyama vingine vinavyopinga mpango wa Serikali wa ubanaji matumizi vimeshatangaza waziwazi kujitoa kwenye mazungumzo hayo iwapo chama cha New democracy kitaendelea kuunga mkono sera ya ubanaji matumizi.

wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema kuwa iwapo Serikali mpya inataka ifanikiwe ni lazima chama Syriza na vyama vingine vilivyopata viti bungeni vijumuishwe kwenye serikali ya muungano vinginevyo hakutakuwa na Serikali imara.