LONDON-UINGEREZA

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Burma, Aung San Suu Kyi, ziarani nchini Uingereza

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Burma Aung San Suu Kyi
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Burma Aung San Suu Kyi REUTERS

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Burma, Aung San Suu Kyi anatarajiwa kuwasili nchini Uingereza muda mchache ujao ambapo anatarajiwa kukutana na familia ya Malkia kabla ya kuhutubia bunge la nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Ziara hiyo ya Suu Kyi ni ya kwanza kuifanya barani Ulaya toka kuachiliwa huru ambapo anatarajiwa kufanya ziara kwenye mataifa karibu matano ya bara la Ulaya na kukutana na viongozi wa mataifa hayo.

Ziara yake ya kwanza aliifanya nchini Norway kwenye jiji la Oslo ambapo alihudhuria sherehe za kukabidhiwa zawadi yake ya tuzo la Nobel aliyozawadiwa miaka ya 90 kwa umahiri wake wa kupigania haki za wananchi wa Burma.

Kwenye ziara yake nchini Uingereza, Suu Kyi atakutana na Prince Charles kabla ya kuhutubia chuo kikuu cha uchumi cha mjini London na baadae kupata fursa ya kuhutubia bunge la nchi hiyo.

Ziara hizo za kiongozi mkuu wa upinzani nchini Burma imekuja kufuatia mabadiliko ya kidemokrasia yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo chini ya utawala wa kiraia wa rais Thein Sein aliyechukua madaraka toka kwa utawala wa kijeshi.