CAIRO-MISRI

Marekani yauonya utawala wa kijeshi nchini Misri kuhusu kumpunguzia rais madaraka

Kiongozi wa baraza la kijeshi nchini Misri, Hussein Tantawi
Kiongozi wa baraza la kijeshi nchini Misri, Hussein Tantawi Reuters

Serikali ya Marekani imeuonya utawala wa kijeshi nchini Misri kukubali kurejesha madaraka rasmi kwa utawala wa kiraia mapema iwezekanavyo ili kuzuia mgogoro unaoweza kuibuka.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Marekani imesema kuwa hatua ya utawala wa kijeshi nchini Misri kuendelea kubakia madarakani huku wakipunguza kwa kiasi kikubwa madaraka ya urais ni jambo ambalo halikubaliki kidemokrasia.

taarifa hiyo imeongeza kuwa kufanya hivyo ni kuwanyima haki wananchi wa Misri ambao walishiriki mapinduzi ya kuuong'oa utawala wa Hosni Mubarack uliokuwa ukiwanyima haki wananchi kutoa madaraka makubwa kwa jeshi la nchi hiyo.

Hapo jana baraza la kijeshi nchini humo lilitangaza kuwa litaachia madaraka kwa rais mwishoni mwa mwezi huu lakini halitampa mamlakarais kurekebisha sheria wala kutunga sheria mapaka idhini ya baraza hilo.

Mohammed al-Assar ni mmoja wa majenerali kwenye baraza la kijeshi na hapo jana alithibitisha baraza hilo kupunguza baadhi ya mamlaka ya rais ikiwemo bajeti ya jeshi ambayo wamesema itaendelea kuamuliwa na jeshi na si bunge wala rais.

Chama cha Muslim Brotherhood nchini humo ambacho jana kliendelea kujitangazia ushindi kwenye uchaguzi wa rais wa duru ya pili kimeitisha maandamano ya nchi nzima kupinga uamuzi wa baraza la kijeshi kutaka kuwanyang'anya mapinduzi yao.

Kiongozi wa chama hicho ambaye amegombea nafasi ya urais Mohammed Mursi amesema kuwa chama chake kamwe hakitakaa kimya na kuacha baraza la kijeshi kuiba mapinduzi yaliyohusisha wananchi wa Misri na kwamba mamlaka ya kuunda katiba na kutunga sheria ni ya rais na bunge na sio baraza la kijeshi.

Kufuatia uamuzi wa baraza la kijeshi na ule wa chama cha Muslim Brotherhood kumezuka hofu ya kiusalama nchini humo ikiwemo kuibuka kwa vurugu kama za wakati wa mapinduzi ya kuuong'oa utawala wa Hosni Mubarack.