LOS CABOS-MEXICO

Rais Barack Obama na rais Vladmir Putin wataka kusitishwa kwa machafuko nchini Syria

Rais wa Urusi Vladmir Putin (kushoto) akiwa na rais wa Marekani Barack Obama (kulia)
Rais wa Urusi Vladmir Putin (kushoto) akiwa na rais wa Marekani Barack Obama (kulia) Reuters

Rais wa Urusi Vladimir Putin na rais wa Marekani Barack Obama wamekutana kwa mazungumzo nchini Mexico wanakohudhuria mkutano wa nchi za G20 na kutaka kusitishwa kwa machafuko nchini Syria.

Matangazo ya kibiashara

Kwenye mazungumzo yao, rais Obama amesema kuwa nchi yake inasikitishwa na kile kinachoendelea kushuhudiwa nchini Syria na kuitaka nchi ya Urusi kuungana na Umoja wa Mataifa katika kutekeleza maazimio makali dhidi ya utawala wa Syria.

Rais Obama ameongeza kuwa iwapo nchi za Urusi na China pamoja na Iran zitaunga mkono maazimio yaliyopitishwa na Umoja wa Mataifa kutaka kuchukuliwa kwa hatua kali dhidi ya Syria, basi machafuko yanayoendelea huenda yakamalizika.

Kwa upande wake rais wa Urusi Vladmir Putin amesema kuwa nchi yake pia inasikitishwa na kile kinachotokea nchini Syria lakini akasita kuunga mkono maazimio yoyote ambayo yataruhusu kutumika kwa nguvu za kijeshi nchini humo.

Rais Putin ameongeza kuwa ni lazima njia ya kidemokrasia itumike katika kutatua mgogoro wa Syria na sio kutumia nguvu wala vitisho kwa utawala wa rais Bashar al-Asad ili aondoke madarakani.

Kiongozi huyo pia amemtamkia waziwazi rais Obama kuhutu nchi yake kutuhumiwa kuwafadhili waasi kwa silaha na kusema kuwa kufanya hivyo ni kuendelea kuchochea machafuko ambayo yanaendelea kushuhudiwa.

mazungumzo ya viongozi hao yanafanyika wakati kiongozi wa msafara wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Robert Mood akitangaza kusitishwa kwa operesheni zote kutokana na kuwa katika hatari ya kushambuliwa.