LONDON-UINGEREZA

Julian Assange akimbilia ubalozi wa Ecuador nchini Uingereza kuomba hifadhi ya kisiasa

Mwanzilishi na mmiliki wa mtandao wa Wikilieaks, Julian Assange
Mwanzilishi na mmiliki wa mtandao wa Wikilieaks, Julian Assange Reuters/Andrew Winning

Mmiliki wa mtandao wa habari chokonozi wa 'Wikileaks', Julian Assange amekimbilia kwenye ubalozi wa Ecuador kuomba hifadhi ya kisiasa kuhofia kukamatwa na kurejeshwa nchini Sweden.

Matangazo ya kibiashara

Assange anakabiliwa na mashtaka ya ubakaji dhidi ya wanawake wawili nchini Sweden ambao walifungua kesi dhidi ya kiongozi huoy wakidai aliwadhalilisha kijinsia mwaka 2010 alipofanya ziara nchini humo tuhuma ambazo Assange mwenye amekana kuhusika.

Juma moja lililopita mahakama kuu ya mjini London ilitupilia mbali rufaa ya mawakili wa Assange ambao walikuwa wanapinga mteja wao kupelekwa nchini Sweden kwenda kukabiliana na tuhuma zinazomkabili jambo ambalo Assange amelipinga.

Akizungumza kwa njia ya simu toka kwenye ubalozi wa Ecuador Assange amesema kuwa ameamua kuomba hifadhi ya kisiasa kwenye ubalozi huo baada ya kuona kuwa kuna uwezekano mkubwa wa yeye kupelekwa nchini Sweden anakodai hatotendewa haki.

Taarifa za kuwepo kwenye ubalozi wa Ecuador zimethibitishwa pia na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ecuador Ricardo Patino ambaye amekiri rais wa nchi hiyo kupokea barua ya Assange akiomba kupatiwa hifadhi ya kisiasa.

Kiongozi huyo wa mtandao wa Wikileaks amekuwa akidai kutishiwa maisha yake na maofisa usalama wa Marekani ambao wamekuwa wakidai ametoa siri kubwa za nchi hiyo kuhusu mipango yake.