CAIRO-MISRI

Maelfu ya wananchi wa Misri waendelea kupiga kambi kwenye uwanja wa Tahrir kupinga utawala wa kijeshi

Maelfu ya wananchi wakiwa kwenye uwanja wa Tahrir kupinga utawala wa kijeshi
Maelfu ya wananchi wakiwa kwenye uwanja wa Tahrir kupinga utawala wa kijeshi Reuters

Maelfu ya wananchi wa Misri wameandamana kwenye uwanja wa Tahrir mjini Cairo wakipinga madaraka mapya ambayo baraza la kijeshi nchini humo limejitangazia huku wakipunguza madaraka makubwa ya rais atakayeteuliwa. 

Matangazo ya kibiashara

Maandamano hayo yanafanyika wakati ambapo tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo bado haijatangaza matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais uliofanyika mwishoni mwa juma lililopita.

Wagombea wote wawili waliokuwa wanachuana kwenye uchaguzi huo, Mohammed Mursi toka chama cha Muslim Brotherhood na Ahmed Shafiq aliyekuwa waziri mkuu kwenye serikali iliyoangushwa wamedai kuibuka na ushindi kwenye uchaguzi huo ambao bado umegubikwa kiza kinene kuweza kujua nani mshindi.

Wafuasi wa Mursi wameendelea kudai kuwa mgombea wao ameshinda uchaguzi huo kwa asilimia 52 na hivyo kura zimetosha kumuwezesha kutangazwa mshindi, tangazo ambalo upinzani nao umelipinga vikali.

Maandamano ya kwenye uwanja wa Tahrir mbali na kupinga madaraka waliojipa utawala wa kijeshi pia wanashinikiza kutangazwa kwa matokeo ya urais ambayo wanaamini mgombea wa chama cha Muslim Brotherhood ameibuka mshindi.

Viongozi wa utawala wa kijeshi nchini Misri umetangaza kuwa utakabidhi madaraka mwisho wa mwezi huu kwa rais mteule huku wakimpunguzia madaraka makubwa kwenye Serikali itakayoundwa.

Wakati maandamano hayo yakifanyika kumeibuka taarifa zinazokinzana kuhusu afya ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Hosni Mubarack ambaye alihukumiwa kifungo cha maisha jela.

Ripoti toka kwenye hospitali alikolazwa kiongozi huyo zinasema kuwa amefariki dunia huku wengine wakidai kuwa hali yake kiafya imeedhoofu sana.