NEW YORK

Mood akiri waangalizi wa Umoja wa Mataifa kushambuliwa nchini Syria

Kiongozi wa msafara wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Robert Mood
Kiongozi wa msafara wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Robert Mood REUTERS/Khaled al-Hariri

Kiongozi wa msafara wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Jenerali Robert Mood ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa walilazimika kusitisha operesheni zao baada ya kulengwa zaidi ya mara tano.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na nchi wanachama wa baraza la usalama Mood amesema kuwa hivi karibuni wamekuwa wakishambuliwa na makundi ya wananchi ambao walikuwa wakiwapokea kwenye miji waliokuwa wakitembelea na kuhatarisha maisha yao.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa mbali na kushambuliwa na watu ambao wamekuwa wakiwapokea waangalizi hao pia wamekuwa wakishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana na kuendelea kufanya kazi yao kuwa ngumu.

Mood ameongeza kuwa wao kama waangalizi hawana nia ya kuendelea kukaa kushuhudia watu wakipoteza maisha kutokana na machafuko yanayoendelea lakini hawana budi kusistisha operesheni zao kutokana na kukosa usalama wa kutosha.

Amekiri pia hawatoondoka nchini humo kwa sasa mpaka pale pengine hali ya mambo itakaporejea kwenye hali ya kawaida kwa wao kuweza kupata nafasi nyingine ya kutembelea maeneo zaidi.

Wakati waangalizi hao wakisitisha operesheni zao, kumeripotiwa kutokea mashambulizi zaidi kwenye mji wa Homs ambao hapo jana Jenerali Robert Mood alisema wananchi wengi wamenaswa kwenye mapigano.