ISLAMABAD-PAKISTAN

Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari, amtangaza Makhdoom Shahabuddin kuwania nafasi ya uwaziri mkuu

Makhdoom Shahabuddin kiongozi aliyeteuliwa kuwania nafasi ya uwaziri mkuu wa Pakistan
Makhdoom Shahabuddin kiongozi aliyeteuliwa kuwania nafasi ya uwaziri mkuu wa Pakistan Reuters

Rais wa Pakistan, Asif Ali Zardari amemtangaza aliyekuwa waziri wa viwanda Makhdoom Shahabuddin kuwa waziri mkuu mpya akichukua nafasi ya Yusuf Raza Gilan aliyeondolewa kwenye nafasi hiyo kwa amri ya mahakama.

Matangazo ya kibiashara

Makhdoom Shahabuddin ambaye anatoka kwenye muungano wa vyama ambavyo vinaunda serikali anachukua nafasi hiyo wakati akikabiliwa na changamoto nyingi endapo bunge litamuidhinisha.

Awali kabla ya uteuzi wake, rais Zardari alikuwa na wakati mgumu wa kuteua jina la waziri mkuu moya baada ya mazungumzo ya saa kadhaa na viongozi ambao wanajumuishwa kwenye serikali ya muungano.

Chama tawala cha Pakistan Peoples kimekuwa kikijipatia umaarufu mkubwa wakati wa utawala wa waziri Gilani kutokana na utendaji kazi wake na kuwa na msimamo pale mahakama inapokuwa inaingilia kati.

Hata hivyo kiongozi huyo anatarajiwa kupata upinzani toka chama kikuu cha upinzani cha Pakistan Muslim League ambacho nacho kitatangaza jina la kiongozi ambaye atachuana na Shahabuddin kwenye uchaguzi wa wazi kabla ya bunge kumuidhinisha.

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa hata kama upinzani utapinga jina lililopelekwa bungeni na rais Zardari, bado chaguo lake linapewa nafasi kubwa ya kuweza kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.