TAHRIR-MISRI

Tume ya uchaguzi nchini Misri yasitisha kutangaza matokeo ya urais

Wafuasi wa chama cha Muslim Brotherhood wakichoma moto picha ya Ahmed Shafiq
Wafuasi wa chama cha Muslim Brotherhood wakichoma moto picha ya Ahmed Shafiq REUTERS/Mohamed Abd El Ghany

Tume ya taifa ya uchaguzi nchini Misri imeahirisha kutangaza matokeo ya urais kufuatia uchaguzi wa duru la pili uliofanyika nchini humo juma moja lililopita. 

Matangazo ya kibiashara

Hapo jana jioni tume ya taifa ya uchaguzi ilitarajiwa kutangaza matokeo ya urais ambayo yalikuwa yanasubiriwa na maelfu ya wananchi wa Misri ambapo wafuasi chama cha Muslim Brotherhood wanadai mkgombea wao Mohammed Mursi ameibuka mshindi.

Wakati kambi ya chama cha Muslim Brotherhood ikidai mgombea wao kuibuka mshindi kwenye uchaguzi wa duru ya pili, wafuasi wa waziri mkuu wa zamani kwenye utawala ulioangushwa Ahmed Shafiq nayo inadai kuwa mgombea wao ameibuka mshindi.

Kutotangazwa kwa matokeo hayo ya urais kumeendelea kuingeza hali ya sintofahamu nchini humo na kuhofiwa kutokea kwa machafuko ambayo yanaweza kusababisha nchi hiyo kuingia kwenye vurugu za wakati wa mapinduzi.

Chama cha Muslim Brotherhood kimewataka wafuasi wake kuendelea kufurika kwenye uwanja wa Tahrir kushinikiza baraza la kijeshi kuachia madaraka kwa rais mteule pamoja na kutaka tume ya taifa ya uchaguzi kutangaza matokeo.

Tume ya taifa ya uchaguzi pamoja na kushindwa kutangaza matokeo ya urais pia haijatangaza rasmi ni lini matokeo hayo yatatangazwa na kuendelea kuzusha hofu ya kutokea machafuko ikiwa yatatangazwa vinginevyo.

wakati huohuo bado hakuna taarifa rasmi kuhusu afya ya Hosni Mubarack ingawa mawakili wa kiongozi huyo wanadai anatumia mashine kupumulia.