ISLAMABAD-PAKISTAN

Chama tawala nchini Pakistan chamtangaza Raja Pervez Ashraf kuwania nafasi ya uwaziri mkuu

Raja Pervez Ashraf, kiongozi aliyeteuliwa na chama cha PPP kuwania nafasi ya uwaziri mkuu
Raja Pervez Ashraf, kiongozi aliyeteuliwa na chama cha PPP kuwania nafasi ya uwaziri mkuu Reuters

Chama tawala nchini Pakistan cha Pakistan Peoples kimemtangaza Raja Pervez Ashraf kuwa mgombea wa chama hicho kwenye nafasi ya uwaziri mkuu kufuatia uteuzi wa awali kupingwa na mahakama kuu.

Matangazo ya kibiashara

Uteuzi wa jina la Raja Pervez Ashraf, umetangazwa na msemaji wa chama hicho wakati akizuwaambia waandishi wa habari kuhusu uteuzi mpya wa jina ambalo sasa litapigiwa kura na wabunge kuidhinisha kuwa waziri mkuu.

Raja Pervez Ashraf kabla ya kuteuliwa kuwania nafasi hiyo alikuwa akihudumu kwenye wizara ya sayansi ya teknolojia.

Wachambuzi wa mambo wanahofu kuwa huenda mahakama ikaibua hoja nyingine kupinga uteuzi wa mgombea huyo kutokana na kashfa za rushwa zilizokuwa zikimkabili wakati akihudumu kwenye wizara ya nishati na maji.

Siku ya Jumatano rais wa Pakistan Asif Ali Zardari alitangaza jina la Makhdoom Shahabuddin aliyekuwa waziri wa viwanda kushika wadhifa huo lakini uteuzi wake uligonga mwamba kufuatia mahakama kuu nchini humo kuagiza kukamatwa kwa kiongozi huyo.

Makhdoom Shahabuddin anatuhumiwa kwa kushiriki vitendo vya rushwa wakati akiwa waziri wa afya jambo ambalo mahakama kuu imesema hana hadhi ya kushika wadhifa wa waziri mkuu mpaka pale atakapobainika hana hatia.

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa siasa za Pakistan zimekuwa zikiingiliwa na mahakama kwa kipindi kirefu jambo ambalo wanaona ni lazima katiba ya nchi hoyo ibadilishwe ili kupunguza madaraka makubwa ya Mahakama kuingilia masuala ya siasa.