KHARTOUM-SUDAN

Maandamano ya kupinga bajeti ya kubana matumizi nchini Sudan yaingia siku ya sita

Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir
Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir REUTERS/Stringer

Polisi kwenye mji wa Khartoum nchini Sudan wametumia mabomu ya mchozi na risasi za mpira kuwatawanya maelfu ya wananchi waliokuwa wanaandamana kwenye mji huo kupinga mpango wa Serikali wa kubana matumizi.

Matangazo ya kibiashara

Maandamano hayo yameingia siku yake ya sita hii leo ambapo wananchi wameendelea kujitokeza wakiwa na mapanga pamoja na mikuki wakishinikiza kujiuzulu kwa Serikali ya rais Omary al-Bashir.

Viongozi wa upinzani nchini humo wamewataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi barabarani kupinga hatua ya Serikali ya kubana matumizi ambayo wamesema itashuhudia maelfu ya vijana wakipoteza ajira zao na gharama za maisha kupanda.

Saata Ahmed al-Haj ni kiongozi wa muungano wa vyama vya upinzani nchini Sudan, ambapo amesema kuwa hatua ya Serikali kubana matumizi kwenye bajeti yake inalenga kuwaumiza wananchi ambapo pia bidhaa muhimu zitaendelea kupanda bei.

Upinzani umepanga kuendelea na maandamano hayo hadi pale rais Bashir atakapong'atuka madarakani ama vinhinevyo akubali kufanyia marekebisho bajeti ya Serikali.

Waziri wa fedha nchini humo juma lililopita alitangaza bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/2013 ambapo alitangaza Serikali kuchukua hatua za ubanaji matumizi ili kukabilina na mdororo wa kiuchumi ambao umeanza kulikumba taifa hilo.

tayari Serikali imepiga marufuku kufanyika kwa maandamano yoyote kwenye mji wa Khartoum.