KABUL-AFGHANISTAN

Watu 11 wamepoteza maisha nchini Afghanistan kwenye tukio la utekaji nyara katika hoteli moja mjini Kabul

Askari wa Serikali ya Afghanistan wakiwa kwenye doria baada ya kufanikisha uokozi
Askari wa Serikali ya Afghanistan wakiwa kwenye doria baada ya kufanikisha uokozi Reuters

Watu kumi na moja wamepoteza maisha nchini Afghanistan na wengine kadhaa wamejeruhiwa baada ya wanamgambo wa Taliban kuteka hoteli moja ya kitalii mjini Kabul.

Matangazo ya kibiashara

Wanamgambo hao wapatao zaidi ya kumi na mbili waliteka hoteli ya Spozhmai na kuwakamata raia wa kigeni waliokuwa wamepumzika kwenye hoteli hiyo kabla ya wanajeshi wa Serikali kuanza hatua za uokozi.

Mapigano hayo yalidumu kwa saa 12 ambapo wanajeshi wa Serikali kwa kushirikiana na wanajeshi wa majeshi ya NATO walifanikiwa kuwaua wanamgambo kadhaa na kisha kuwaokoa baadhi ya mateka.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani wa nchi hiyo, Sediq Sediqqi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa wapiganaji hao walikuwa wamevalia vifaa vya mlipuko lakini hakuna hata mmoja ambaye alifanikiwa kujilipua.

Awali kabla ya shambulio hilo, msemaji wa kundi la Taliban alisema kuwa wameua watu nane ambao hawakuwa raia bali ni wanajeshi wa Serikali jambo ambalo hata hivyo Serikali imekanusha kutokea mauaji hayo.