JAMUHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO.

Wananchi mashariki mwa DR Congo wadai kunyanyaswa na wapiganaji

Jamii zilizopo Kivu ya mashariki nchini DR Congo zimelalamika kunyanyaswa na wapiganaji waasi
Jamii zilizopo Kivu ya mashariki nchini DR Congo zimelalamika kunyanyaswa na wapiganaji waasi AFP/ MARC HOFFER

Wananchi waishio vijiji vya Ufamando na Katoyi,katika mtaa wa Masisi huko mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasi ya congo, wamelalamika juu ya usalama wao kwa kile wanachosema kuwa wamekuwa wakikabiliana na manyanyaso yanayofanywa na makundi ya wapiganaji maimai ambayo yamezidi katika eneo hilo.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa hii imethibitishwa na naibu mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa ahusikaye na masuala ya haki za binadamu nchini Congo,Bibi Leila Zerugui ambaye amesikitishwa na hali ya usalama inavyozidi kudhorota mashariki mwa nchi hiyo.
Imearifiwa kuwa kumekuwepo na makundi ya wapiganaji maimai ambayo yanalaumiwa kwa kuwanyanyasa wananchi katika miji na vijiji kadhaa huko mashariki mwa Congo,hasa katika mtaa wa Masisi,mkoani Kivu ya Kaskazini.

Kidole cha lawama kimeelekezwa dhidi ya kundi la wapiganaji maimai Raia Mutomboki ambalo inasemekana linaundwa na watu kutoka makabila mbali mbali ya mtaa wa Masisi katika Kivu ya kaskazini na mengine makabila kutoka Kivu kusini.

Semahane Mihigo,mwenyekiti wa kongamano kuu la Lindi,ametoa mwito kwa maafisa wakuu wa jeshi la serikali kutuma wanajeshi kwa masharti kuwa hawatopokea tena wanajeshi waliotokea katika makundi ya waaasi wa zamani.

Katika hatua nyingine Bibi Leila Zerugui amekanusha taarifa kuwa tume ya umoja wa mataifa huko DRC inawaunga mkono wapiganaji waasi wa Rwanda wa FDLR mashariki mwa nchi hiyo.