DAMASCUS-SYRIA

Baada ya Assad kukiri nchi kuwa katika hali ya vita, kituo cha TV chashambuliwa

RFI

Mtu mmoja mwenye silaha ameingia katika eneo la kituo cha televisheni inayounga mkono serikali ya Rais Bashar al-Assad nchini Syria na kushambulia kwa risasi na kuua wafanyakazi watatu wa kituo hicho. 

Matangazo ya kibiashara

Baada ya kushambulia kwa risasi mtu huyo alirusha bomu na kulipua kituo hicho cha Ikhbariya kilichopo kilomita 20 kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Damascus.

Hata hivyo kituo hicho kimerejesha matangazo yake na kilionyesha picha za majengo yaliyoharibiwa kutokana na shambulio hilo huku damu ikionekana kutapakaa katika eneo la tukio.

Shambulio hilo linakuja huku Rais wa Syria Bashar Al Assad kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miezi kumi na mitano akikiri nchi yake ipo kwenye hali ya kivita na kulitaka Baraza lake jipya la Mawaziri kuhakikisha wanashinda vita hivyo.

Rais Assad amesema kila upande wa nchi hiyo umeendelea kukabiliwa na kushuhudia mashambulizi yanayofanyika katika taifa hilo kitu ambacho kimesababisha uwepo wa vifo vya raia kila uchao.

Kauli hii inakuja wakati ambapo nchi zenye nguvu duniani zikiendelea kutofautiana juu ya hatua za kuchukua dhidi ya nchi ya Syria na hapa Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa UN Vitaly Churkin anasema mapendekezo ya Kofi Annan yanstahili kutekelezwa.

Katika hatua nyingine Wanaharakati nchini Syria wamesema kuwa watu mia moja na kumi na sita wamepoteza maisha kati yao sitinina wanane wakiwa raia na arobaini na mmoja ni wanajeshi.