DRC-RWANDA-MAREKANI

Marekani yaitaka Rwanda kuacha kufadhili na kuwahifadhi waasi wanaopambana na serikali ya DRC

Wanajeshi wa Serikali ya DRC wakiwa Mashariki mwa nchi hiyo kwa ajili ya kuwasaka wapiganaji wa M23
Wanajeshi wa Serikali ya DRC wakiwa Mashariki mwa nchi hiyo kwa ajili ya kuwasaka wapiganaji wa M23

Marekani imeitaka serikali ya Rwanda kuacha mara moja kuendelea kuwafadhili na kuwahifadhi waasi wanaopambana na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kufuatia uchunguzi wa Umoja wa Mataifa UN kuonesha maofisa wa serikali ya Kigali wanahusika.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa ambayo imetolewa na serikali ya Marekani imesema wakati umefika kwa Rwanda kuacha kabisa kujihusisha kwa namna yoyote ile kuwafadhili waasi hao ambao wameendelea kupambana na serikali na kuchangia maelfu ya wananchi kukimbia nchi za jirani.

Marekani imetoa taarifa hii ya kuionya Rwanda kuacha kuendelea kufadhili waasi wanaopambana na serikali ya DRC baada ya ripoti ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa UN kuonesha waasi wa kundi la M23 wanafadhiliwa na wengine kuhifadhiwa chini ya ardhi ya Kigali.

Huu ni ujumbe wa kwanza kutoka serikali ya Marekani kuelekezwa kwa Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye amekuwa rafiki mkubwa wa nchi hiyo lakini mwenyewe amekuwa akikana kuhusika kwa namna yoyote kwenye vita ya DRC.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani Victoria Nuland kupitia barua pepe yake amesema wanafanyiakazi ushahidi ambao umekusanywa na Umoja wa Mataifa UN juu ya tuhuma za ufadhili wa waasi wa M23 unaofanywa na serikali ya Rwanda.

Nuland anaweka bayana wakati wakiendelea kufanyiakazi ushahidi huo wanaitaka Rwanda kuacha kujishughulisha kwa namna yoyote na kuwafadhili waasi wa M23 wanaotajwa kuongozwa na Mbabe wa Kivita anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC.

Kauli ya Marekani inakuja wakati ambapo Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu ikiwemo Amnesty International yakitoa wito kwa Umoja wa Mataifa UN na wafadhili wa Rwanda kuchukua hatua ili kudhibiti ufadhili na uhifadhi wa waasi wa M23 wanaotajwa kupata mafunzo huko Kigali.