MALI-UFARANSA

Mali yazua mjadala mzito ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN na Bungeni Ufaransa

Wapiganaji wa Kundi la Ansar Dine la nchini mali ambalo limekuwa likifanya mashambulizi na kuzua hofu ya usalama
Wapiganaji wa Kundi la Ansar Dine la nchini mali ambalo limekuwa likifanya mashambulizi na kuzua hofu ya usalama Reuters/Adama Diarra

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN limeketi kujadili pendekezo la kupitisha azimio lenye lengo la kudhibiti machafuko ambayo yanaendelea kushika kasi nchini Mali huku Ufaransa ikiwa na imani suala hilo litafanikiwa.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesema Baraza la Usalama linanafasi kubwa ya kuhakikisha amani na utulivu unapatikana nchini mali kutokana na kuendelea kushuhudia mapigano yakichacha Kaskazini mwa nchi hiyo.

Kauli ya Fabius imekuja baada ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle na kusema azimio hilo ndiyo suluhu pekee ambayo itasaidia kurejesha hali ya usalama katika taifa hilo.

Fabius bila ya kutafuna maneno amesema azimio hilo halitakuwa na msingi iwapo majirani wa Mali hawatokuwa tayari kushiriki kwenye mpango huo wa kurejesha utulivu na kuzua vifo vya wananchi wasio na hatia.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault akihutubia Bunge la Ufaransa amesema kile ambacho kinashuhudiwa Timbuktu ni ishara tosha kabisa kuwa eneo hilo linakabiliwa na hali mbaya ya kiusalama.

Katika hatua nyingine Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS imesema wanajeshi wao elfu tatu na mia tatu wapo tayari kupelekwa nchini Mali ili kushika doria katika taifa hilo ikiwa chini ya serikali ya mpito.

Naye Rais wa Guinea Alpha Conde amesema serikali ya umoja inayoongoza nchi hiyo ndiyo ina uhalali wa kuomba majeshi ya nje yaweze kuingia katika nchi hiyo kushika doria na kusaidia ulinzi.