PAKISTAN-AFGHANISTAN-MAREKANI

Pakistan yafungua mipaka yake kuruhusu zana za kijeshi za NATO zipelekwe nchini Afghanistan

Baadhi ya malori ya mafuta ya Jeshi la NATO takiwa yamezuiliwa kupita nchini Pakistan kabla ya kuruhusiwa na serikali
Baadhi ya malori ya mafuta ya Jeshi la NATO takiwa yamezuiliwa kupita nchini Pakistan kabla ya kuruhusiwa na serikali REUTERS/Athar Hussain/Files

Serikali ya Pakistan imeridhia hatua ya kufungua mipaka yake kwa ajili ya kuruhusu misaada na zana mbalimbali kuelekea nchini Afghanistan kitu ambacho kimemaliza mvutano uliokuwepo baina ya nchi hiyo na Marekani. Pakistan imefikia hatua ya kufungua mipaka yake kuruhusu upitishwaji wa zana za kijeshi za Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO kipindi hiki ambapo Marekani imeomba radhi kutokana na kuchangia vifo vya wananchi.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton amekiri nchi yake imekuwa ikifanya makosa kutokana na kusababisha kutokeza kwa vifo vya wananchi wasio na hatia kutokana na mashambulizi ya ndege zake za kivita.

Taarifa kutoka nchini Marekani zinasema kuwa sehemu ya makubaliano baina ya nchi hizo mbili imeifanya serikali ya Washington kuachia dola bilioni 1.1 kusaidia jeshi la Pakistan liweze kuendelea na operehseni zake za ulinzi.

Fedha hizo zilikuwa zinashikiliwa kwa sababu ya uwepo wa hali ya kutokuelewana baina ya pande hizo mbili kutokana na kushindwa kuafikiana juu ya kufunguliwa kwa njia za kupitisha zana za kijeshi kwenda Afghanistan.

Makubaliano hayo yametamatisha miezi saba ya hali tete ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya Marekani na Pakistan ambao ulitetereka zaidi baada ya kuuawa kwa Kiongozi wa Al Qaeda Osama Bin Laden.

Pakistan imekuwa ikituhumiwa kwa kiasi kikubwa kuwa hifadhi ya kudumu kwa magaidi huku mfano ukiwa ni kukuawa kwa Osama kwenye operesheni ya kijeshi ya makomandoo wa Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Clinton ametangaza kufunguliwa kwa mipaka ya Pakistan baada ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Islamabad Hina Rabban Khar na kuafikiana baada ya kujadiliana kwa miezi miwili.