JAPAN

Janga la kuvuja kwa mionzi ya nyuklia huko Fukushima labainika ni la kutengenezwa na binadamu

Kinu cha kuzalisha nyuklia nchini Japan cha Fukushima ambacho mionzi yake ilivuja baada ya kutokea kwa Tsumani
Kinu cha kuzalisha nyuklia nchini Japan cha Fukushima ambacho mionzi yake ilivuja baada ya kutokea kwa Tsumani REUTERS/Issei Kato

Mkasa wa kuvuja kwa mionzi ya nyuklia nchini Japan kutoka kwenye kinu cha Fukushima mwaka mmoja uliopita umebainika kuwa ni janga ambalo limetengenezwa na binadamu na halikuchangiwa na tetemeko la chini ya bahari Tsunami kama ilivyokuwa inaelezwa. Jopo lililoundwa na Bunge nchini Japan limebainisha hilo kwenye ripoti yake baada ya kufanya uchunguzi wa kina kubaini madai yaliyokuwepo awali ya kwamba janga hilo la kuvuja kwa mafuta limechangiwa na Tsunami.

Matangazo ya kibiashara

Matokeo ya Uchunguzi huo yanaonesha uwepo wa kutokuelewana baina ya Serikali na Shirika la TEPCO ambalo linasimamia masuala ya nyuklia na kitu ambacho kilichangia pakubwa kila upande kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Uchunguzi huo umesema kile ambacho kimefanyika ni usaliti kwa Taifa na hivyo kuchangia kuzuka kwa janga hilo la kuvuja kwa nyuklia na hivyo wamehitimisha kwa kusema ni janga ambalo limetengenezwa na binadamu.

Jopo hilo bila ya kung'ata maneno limesema kuwa wanaamini chanzo cha tatizo hilo ni Shirika la TEPCO kushindwa kupata masaada unaofaa kutoka kwenye mfumo wa Utawala na hivyo kuibuka kwa tatizo hilo.

Uchunguzi huu unaanza kuondoa wingu zito ambalo limekuwa likitanda tangu kutokea kwa janga la kuvuja kwa mionzi ya nyuklia nchini Japan kitu ambacho kilichangia hata baadhi ya vyakula vyake kupigwa marufuku kutumika.

Kabla ya kutolewa ripoti ya uchunguzi huu Shirila hilo la Umeme na nyuklia la TEPCO lilijisafisha na kusema kuvuja kwa mionzi ya nyuklia kulichangia kwa kiasi kikubwa na ukubwa wa tetemeko la chini ya bahari lililopiga nchi hiyo mwaka jana.

Ripoti hii ya Bunge inaweza ikatumika vizuri katika kuhakikisha wanachukua hatua dhidi ya wale wote ambao wamehusika kwenye uzembe ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kuvuja kwa mionzi hiyo ya nyuklia kutoka kinu cha Fukushima.