RWANDA-DRC

Rais Paul Kagame wa Rwanda akanusha kuwafadhili Waasi wa M23 wanaopambana na Serikali ya DRC

Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye amekanusha serikali yake kushiriki kuwafadhili waasi wanaopambana na serikali ya DRC
Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye amekanusha serikali yake kushiriki kuwafadhili waasi wanaopambana na serikali ya DRC © AFP/Thomas Samson

Serikali ya Rwanda imeendelea kukanusha kuhusika kwa namna yoyote kufadhili na kuwahifadhi waasi wa Kundi la M23 linalopambana na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC Mashariki mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema nchi yake haifadhili waasi wa Kundi la M23 kwa kuwapa silaha au kuwapa mafunzo kama ambavyo imekuwa ikielezwa na Umoja wa Mataifa UN kupitia kwenye ripoti zao.

Rais Kagame amesema hizo ripoti ambazo zimekuwa zikitolewa kila kukicha na kuitaja nchi yake kuwafadhili na kuwahifadhi waasi wa M23 zimesheheni uongo na hakuna uthibitisho wowote uliopo.

Serikali ya Kigali imesema haihusiki kwa namna yoyote na kutoa mafunzo au kuwapatia silaha waasi wa Kundi la M23 ambalo limekuwa kinara wa kupambana na serikali ya Kinshasa katika eneo la Mashariki.

Rais Kagame amesema wale wenye ushahidi wa kutosha kama nchi yake inawafadhili waasi wanaopambana na Serikali ya DRC wapeleke badala ya watu kuendelea kusikiliza ripoti ambazo zimejaa uongo.

Kagame ameweka bayana kwa muda mrefu wamekuwa wakishirikiana na serikali ya Kinshasa kwa hiyo hawawezi kuthubutu kutoa ufadhili au makazi kwa waasi kwani watakuwa wanahatarisha usalama wa wa nchi ya DRC.

Ripoti ya hivi karibuni ambayo imetolewa na Umoja wa Mataifa UN inaituhumu Rwanda kwa kulifadhili Kundi la Waasi la M23 ambalo linaongozwa na Mbabe wa Kivita Jenerali Bosco Ntaganda ambaye anasakwa na Mahakam ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita ICC.

Ripoti ya UN inakwenda mbali zaidi na kusema Rwanda imekuwa mstari wa mbele kuwapa fedha, wanawaunga mkono kisiasa, wanawapa nguvu kazi pamoja na silaha ambazo vyote vinagharamiwa na serikali ya Rwanda.